DP kufuta kikokotoo cha wastaafu

CHAMA Cha Democratic Party (DP) kimesema serikali yake itaboresha mafao ya wastaafu.

Mgombea urais kupitia chama hicho, Abdul Juma Mluya amesema hayo katika mkutano wa kampeni katika uwanja wa stendi ya zamani mjini Tabora.

Mluya amesema Serikali ya DP itafuta kikokotoo kinachotumika sasa kulipia wastaafu akidai kuwa hakiwasaidii.

Pia amesema falsafa ya DP ni kulinda haki, usawa na masilahi ya wananchi hivyo kama watapewa ridhaa ya kushika dola Oktoba 29, mwaka huu ndani ya siku 100 za kwanza atakomesha dhuluma kwa wananchi.

Mluya amesema serikali ya DP itawakopesha nyumba watumishi wote ili watakaostaafu wawe na mahala pa kuishi na wale watakaoshindwa kulipa mikopo ya nyumba zao watalipa kupitia mafao yao.

SOMA: Vyama, wagombea wapewa masharti kampeni Uchaguzi Mkuu

“Serikali ya Chama Cha Democratic Party itawaheshimisha watumishi wote wakiwemo maaskari kwa kuwapa mishahara mizuri ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi mkubwa,” amesema.

Mluya ametaja vipaumbele vingine vilivyoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama chake kuwa ni kuruhusu uraia pacha kwa diaspora ili kuwapa fursa ya kuja kuwekeza nchini sanjari na kuipitia upya mikataba ya madini.

Alitaja vipaumbele vingine ni kusimamia rasilimali za nchi ili zinufaishe wazawa na kudhibiti utoroshaji malighafi nje ya nchi, pia serikali yake itatunga sheria itakayowabana watoto ili watakapokua wakubwa watunze wazazi wao.

Mluya amesema watadhibiti wanunuzi wanaoibia wakulima, watajenga kiwanda cha asali Tabora, kiwanda cha tumbaku kitahamishwa kutoka Morogoro kuja Tabora, wajawazito watajifungua bure na watapiga marufuku hospitali zote kutoza maiti.

Mgombea mwenza wa urais kupitia DP, Saadun Abdulrahman Khatib amesema chama hicho kinatetea masilahi ya wananchi hivyo akaomba wawapigie kura za kutosha ili washike dola.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button