Samia kuifanya Ruvuma kitovu cha biashara

SONGEA : MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema wananchi wakimchagua, Mkoa wa Ruvuma utakuwa kitovu cha biashara. Samia alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni katika Uwanja wa VETA mjini Songea mkoani Ruvuma jana.
Alisema serikali ina mikakati ya kufungua Mkoa wa Ruvuma na Ukanda wa Kusini unaojumuisha mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi uwe wa biashara. Samia alisema serikali yake itajenga kilometa 1,000 za Reli ya Kisasa (SGR) itakayounganisha mikoa ya Mtwara na Ruvuma ili kurahisisha usafirishaji wa madini yatakayochimbwa Mchuchuma na Liganga.
Alisema Kiwanja cha Ndege Songea kimeboreshwa na awamu ya pili ya ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 70. “Nimetua juzi, nimeona njia ya kurukia haipungui kilometa tatu inayoruhusu ndege kubwa kutua hapa Songea. Njia hiyo imeongeza idadi ya miruko ya ndege kutoka 276 hadi miruko 463 na idadi ya abiria kutoka 3,971 hadi abiria 20,667 kwa mwaka,” alisema Samia.
Alisema ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay umefikia asilimia 35 na kwamba serikali imekamilisha ujenzi wa Bandari ya Ndumbi, ambayo imechochea biashara baina ya Tanzania na Malawi kupitia Nkata Bay. Hivyo, kuongeza fursa za kiuchumi Ziwa Nyasa. Samia alisema mwaka jana alizindua Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay inayounganisha Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay.
“Tunafungua ukanda ili biashara ziweze kufanyika kwa anga, barabara, maji, ili Ruvuma iwe kitovu kikubwa cha biashara,” alisema. Samia alisisitiza ahadi ya kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Kidatu – Ifakara – Malinyi hadi Lumecha inayounganisha Ruvuma na Mkoa wa Morogoro ambayo pia itachochea biashara. “Tunafungua ushoroba wa Kusini kwa njia zote, anga, maji, barabara na reli ili kufanya ukanda huu uwe wa kibiashara,” alisema.
Aliongeza: “Kuna maeneo ambayo mawasiliano ya simu siyo mazuri. Hilo nalo tunakwenda kulifanyia kazi kuhakikisha mawasiliano ya simu yawe mazuri, kwa sababu ukanda wa biashara lazima uwe na urahisi wa mawasiliano”.
Huduma za kijamii Samia alisema katika sekta za maendeleo ya jamii ambazo ni maji, elimu, afya na umeme, serikali imetekeleza miradi hiyo kwa kasi kubwa. Alisema katika maji kuna miradi mingi ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya mkoa huo na itakapokamilika, kiwango cha upatikanaji wa maji kitaongezeka na kupita kiwango kilichoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025.
Kuhusu elimu, Samia alisema ujenzi wa madarasa na shule mpya umefanyika na serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo. Ameahidi kujenga na kukamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha Tawi la Songea kitakachokuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 10,000 kwa mkupuo. Pia, alisema serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa chuo cha watu wenye ulemavu eneo la Liganga Jimbo la Peramiho kitakachotoa mafunzo yaliyokusudiwa. Mradi wezeshi kwa ajira Samia alisema serikali imetekeleza mkakati wa nishati safi zaidi ya ilivyotarajiwa katika ilani.
“Ilani ilituambia tukifika 2025 vijiji vyote viwe na umeme lakini serikali ipo katika vitongoji kuunganisha umeme. Kwa sasa nusu ya vitongoji vya Tanzania tayari vimeshaunganishwa na nishati hiyo,” alisema. Aliongeza: “Tunafanya hivyo kwa sababu tuliahidi kila wilaya kuwa na kongani za viwanda na tunataka tutakapoanza kuweka kongani za viwanda, umeme uwe umeshafika na ndiyo maana tunakwenda kwa kasi.” Alitoa mfano wa Mabada, akisema kwamba serikali itaweka viwanda vya kuongeza thamani zao la misitu ili kuongeza ajira na kukuza uchumi kwa vijana na taifa.
Pia, serikali inakusudia kuweka viwanda vya kuongeza thamani kwenye zao la kahawa na parachichi. “Kule Peramiho tumepata mwekezaji mkubwa wa kiwanda cha sukari na shamba kubwa la miwa. Hii pia ni fursa nyingine kutengeneza ajira kwa vijana wetu,” alisema. Kilimo Samia alisema serikali yake itaendelea kuwekeza kwa kuongeza tija ya upatikanaji wa ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo.
Alisema kwa upande wa zao la kahawa ambalo miche na pembejeo za kilimo zinatolewa kwa ruzuku, uzalishaji wake umeongezeka na kwa Mbinga uzalishaji wake umeongezeka maradufu. Aidha, Samia aliahidi kuwa serikali yake itajielekeza kujenga viwanda vya kuongeza thamani ili kuongeza ajira nyingi kwa vijana. Pia, alisema serikali imetekeleza mradi wa ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhia mazao mkoani Ruvuma.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea ina maghala 11, Mabanda tisa, Namtumbo saba na ghala moja kwa Manispaa ya Songea. Samia alisema katika Manispaa ya Songea, serikali itakamilisha ujenzi wa Soko la kisasa Manzese A na B. Madini. Samia aliahidi kuendeleza kutoa kipaumbele uchimbaji salama kwa wachimbaji wadogo. “Tutakwenda kuboresha wachimbaji wadogo lakini pia tutawaelekeza uchimbaji ambao utatunusuru kwenye vifo kwenye migodi ya uchimbaji,” alisema.
Aliongeza: “Niseme pia kwamba, mkoa huu umebarikiwa kuwa na madini mengi kuanzia dhahabu, shaba, makaa ya mawe, madini ujenzi na vito hadi urani yanapatikana ndani ya mkoa huu”. Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa na kipaumbele kikiwa ni katika uchimbaji na wachimbaji wadogo. Pia, alisema wataendelea na mradi wa kuchimba madini ya urani na kuwa lengo la serikali yake ni yachakatwe na yasafishwe ndani ya nchi. SOMA: Wachimbaji wadogo 250 waongezewa ujuzi Geita