NIT Kufunga taa uwanjani kuimarisha mazoezi

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk Prosper Mgaya, amesema uwanja wa michezo wa chuo hicho utafungwa taa ili kuruhusu mazoezi kufanyika muda wowote.
Amesema hayo Septemba 22,2025 wakati wa uzinduzi wa bonanza la michezo kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo, yaliyofanyika chuoni hapo, Dk Mgaya amesema hatua hiyo inalenga kuongeza fursa kwa watumishi na jamii ya NIT kushiriki mazoezi kwa wakati wa mchana na usiku.
“Leo tunaposherehekea historia hii, tunatumia bonanza hili si kwa ajili ya burudani pekee, bali pia kama sehemu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na afya zetu, ili kuongeza ari ya utendaji miongoni mwa watumishi na jamii ya NIT,” amesema.

Ameongeza kuwa afya bora ya watumishi ni chachu ya utendaji bora wa kazi na msingi wa mafanikio ya taasisi.
Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, wavu, kikapu, kuvuta kamba, kufukuza kuku, kukimbia magunia na riadha.
Dk Mgaya pia ameahidi kuchangia kiasi cha Sh milioni 2 kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa bonanza hilo na maandalizi ya sherehe baada ya maadhimisho hayo.

“Kwa kuzingatia matokeo chanya ya mazoezi ya viungo kwa watumishi, ofisi ya mkuu wa chuo itaendelea kumtumia mtaalamu wa mazoezi katika kutoa elimu, ili jamii ijenge tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara. Naomba watumishi wote tushiriki kwa wingi katika mazoezi yanayoratibiwa na Ofisi ya Naibu Mkuu wa Chuo kupitia ofisi ya Utawala na Fedha, ili kudumisha afya zetu,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bonanza, Cornelio Swai amesema licha ya changamoto za ratiba na ufinyu wa bajeti, bonanza hilo limefanikiwa kushirikisha watumishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Naye Makamu wa Chuo hicho, John P. John, amesema timu zote zimejiandaa vyema kwa michezo hiyo kwa kutambua kuwa mazoezi ni afya na msingi wa utendaji bora.



