CCM kuimarisha kilimo biashara

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema serikali yake inataka kukuza kilimo kiwe biashara.

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan amesema hayo kwenye mkutano wa kampeni Ndanda mkoani Mtwara.

Samia amesema Ndanda itaunganishwa na Mji wa Masasi kwa barabara ya lami kurahisisha usafirishaji wa mazao.

“Ahadi yangu ni kwamba, tutaboresha barabara kwa kiwango cha lami na changarawe ndani ya Jimbo la Ndanda na zile za kuifungua Ndanda. Lengo letu ni kuiunganisha Ndanda na Mji wa Masasi, ili mazao yaende kwa haraka sana,” amesema.

SOMA: Samia: Tunajiamini, sera zetu zinaaminika

Samia amepongeza wananchi wa Ndanda kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara.

“Kupitia pembejeo za ruzuku kwa kweli mmetenda haki na uzalishaji umekua. Sasa tutaendelea kutoa ruzuku kwenye pembejeo na pia kuwawezesha kuendelea kuzalisha zaidi, kwa sababu lengo letu ni kufanya kilimo biashara,” amesema.

Ameongeza: “Zamani tulikuwa na mazao tunalima kwa ajili ya chakula pekee, hayakuwa kwenye biashara. Lakini sasa hivi kila tunachozalisha ni biashara, mchele ni biashara, mahindi ni biashara, choroko ni biashara, mbaazi ni biashara, ufuta ni biashara, kwa hiyo lengo letu ni kukuza kilimo biashara.”

Samia amesema serikali itaendelea kuwapa wakulima pembejeo za ruzuku ili wazalishe kwa wingi, wauze na kupata fedha nyingi na serikali ipate mapato, iendelee kutekeleza miradi ya maendeleo zikiwemo barabara, shule na vituo vya afya.

“Najua tumefanya mambo mengi kwenye afya lakini mahitaji bado yapo. Bado kuna zahanati zinatakiwa, bado kuna kata zinahitaji vituo vya afya, kwa hiyo tutaendelea kufanya hivyo ili kila mwananchi popote pale alipo apate huduma,” amesema.

Samia amesema katika sekta ya elimu, ataendelea kutoa elimu bila malipo lakini pia elimu jumuishi, ili watoto wenye mahitaji maalumu waweze kupata elimu.

“Natambua kwamba hapa Ndanda kuna shule maalumu. Niwaahidi tunaenda kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, ikiwa ni pamoja na kujenga karakana ili vijana watoke na ujuzi, ili waweze kujiajiri na kuajiriwa, kujenga uzio na kuwapa gari,” amesema.

Samia amesema miaka mitano iliyopita serikali yake ilijitahidi kutoa Sh bilioni 13 na kutekeleza miradi ya maji 63 na bado miradi mingine inaendelea.

“Natambua katika miradi ile maji yanakuwa machafu, hivyo tumeanza ujenzi wa machujio ya maji na tayari zimeletwa Shilingi bilioni 360 ili wananchi wapate maji safi na salama. Pia, tumekamilisha usanifu kwa ajili machujio mawili, lengo letu ni wananchi wapate maji safi na salama,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button