CCM yaja na mashamba darasa

MUFINDI : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuanzisha mashamba darasa ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.Mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema mashamba hayo ni sehemu ya mkakati wa CCM katika miaka mitano ijayo kuboresha maisha ya Watanzania kwa vitendo, sambamba na ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2025/2030.

Dk Nchimbi alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Ifwagi, Jimbo la Mufindi Kaskazini mkoani Iringa juzi.“Tunakwenda kuanzisha mashamba darasa kwa ajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi wetu. Tunataka kila mmoja akifanya shughuli zake, afanye kwa utaalamu, aweze kupata tija kubwa na maisha yake yawe bora zaidi.

Haya mashamba darasa ndiyo yatakuwa shule ya maendeleo ya vitendo,” alisema. Pia, Dk Nchimbi alitangaza dhamira ya chama hicho kuanzisha vituo vya ukusanyaji na uuzaji maziwa ili kuleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ya vijijini.

Alisema CCM itaendelea kutekeleza mikakati kuhakikisha huduma za jamii kama elimu, afya, maji, barabara na nishati zinaboreshwa zaidi. SOMA: Samia kuwapa raha wakulima, wafugaji

Dk Nchimbi alisema CCM imejidhihirisha ni chama cha watu na chama chenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania. “CCM ndiyo chama pekee Afrika chenye wanachama zaidi ya milioni 13.5 waliosajiliwa kwa mfumo wa kidijiti.

Ni chama kilichojijengea muundo bora unaofika hadi kwa balozi wa nyumba 10. Hakuna chama kingine chenye uimara wa aina hii,” alisema Dk Nchimbi. Alisema wananchi wana kila sababu ya kuendelea kukiamini chama hicho kutokana na utekelezaji wa ahadi za maendeleo ndani ya kipindi cha awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Naye Mgombea ubunge wa Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe alisema ndani ya muda mfupi wamejengewa barabara za lami zaidi ya kilometa 31, vituo vipya vya afya, sekondari mpya na miradi mikubwa ya maji.

“Hatujawahi kupata maendeleo ya kiwango hiki ndani ya muda mfupi. Hii ni dhamira ya kweli ya CCM kupitia Rais Samia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button