Ngajilo: Kura yenu, deni lenu kwangu

IRINGA: Kuelekea kesho, Oktoba 29 siku ya kupiga kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehitimisha rasmi kampeni zake Iringa Mjini, huku mgombea wa ubunge wa chama hicho, Fadhili Ngajilo, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi na mapema kupiga kura kwa amani, ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM.

Akizungumza na wanahabari leo, Ngajilo alisema kampeni zimekwenda vizuri na kwa mafanikio makubwa, kutokana na mapokezi chanya na ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa wananchi wa kila kata, mtaa na kitongoji.

“Naomba niwashukuru wananchi wa Iringa Mjini kwa mapokezi mazuri tuliyoyapata katika kampeni zetu. Tumefanya mikutano ya hadhara, tumetembelea maeneo ya biashara, taasisi za elimu, masoko, maeneo ya ujasiriamali, na hata nyumba kwa nyumba wananchi wametupokea vizuri sana. Sasa tunawaomba kesho mjitokeze kwa wingi kutupigia kura, ili yale tuliyoahidi tuyatekeleze kwa vitendo,” alisema Ngajilo.

Aliongeza kuwa kura za wananchi zitampa nguvu na deni la kufanya kazi kwa bidii kubwa zaidi, akiahidi kuwa sauti ya wananchi bungeni, na kuwa daraja kati yao na taasisi mbalimbali za maendeleo za ndani na nje ya nchi.

“Kura yenu ndiyo itanipa nafasi ya kuwa kiungo cha huduma bora za kijamii, mlezi wa makundi ya wajasiriamali kama machinga, bodaboda na daladala. Pia nitakuwa nguzo ya usalama wa raia na mali zao, pamoja na kupambana na ukatili wa kijinsia na watoto,” aliongeza Ngajilo.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Hassan Makoba, naye alisema chama hicho kimefanya kampeni zake kwa siku 60 mfululizo, ikiwemo mikutano 31 ya hadhara na midogo midogo katika kila mtaa wa manispaa.

“Tunashukuru viongozi wote wa chama, wanachama na wapenzi wa CCM kwa kujitoa. Tumezunguka kila kona ya Iringa, tukiwasikiliza wananchi na kueleza sera zetu. Kesho, vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa mbili asubuhi, hivyo tunaomba tujitokeze mapema na kwa amani kupiga kura,” alisema Makoba.

Amesisitiza kuwa vituo vya kupigia kura vimesogezwa karibu na makazi ya watu ili kurahisisha upigaji kura, akionyesha imani kubwa kuwa CCM itapata ushindi mkubwa kutokana na mwamko na mapokezi mazuri ya wananchi.

“Tumejipanga vizuri, na tunaamini ushindi wa kesho utakuwa mkubwa na wa kihistoria. Baada ya uchaguzi, CCM itatekeleza kwa vitendo kila ilichoahidi katika kampeni hizi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button