Mgera FC yaweka rekodi, yanyakua mil 10/- Vunjabei Cup

IRINGA: Uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege ulilipuka kwa shangwe. Ilikuwa dakika ya 72 tu—dakika inayoweza kuandikwa kwa herufi za dhahabu kwenye historia ya soka la Iringa—wakati mshambuliaji mahiri Mboni Steven alipopiga kombora safi lililozima ndoto za Kising’a FC na kuipa Mgera FC ubingwa wa Vunjabei Cup 2025.

Bao hilo la kiufundi, lililopigwa kwa ustadi wa “striker wa kuzaliwa,” liliifanya timu hiyo kuondoka na kitita cha Sh milioni 10, medali na kombe lililong’aa mithili ya taji la dunia.

Kising’a FC, ambao kwa dakika nyingi walionekana kulidhibiti lango, walilazimika kutuliza maumivu kwa kutwaa Sh milioni 3 na medali.

Wao ni washindi wa pili kwa heshima, lakini maumivu ya bao la Mboni yataendelea kuwasumbua kwa muda mrefu.

Katika mpambano wa kusaka mshindi wa tatu, Kalenga FC waliibuka vinara kwa kuigaragaza BBC FC 2–1, wakionyesha soka safi la kupenya ngome kwa pasi fupi za kupendeza—mtindo uliowapa mashabiki “mzuka” wa kweli wa soka la mtaani.

Fainali hizo hazikuwa tu mechi za mpira; zilikuwa kama tamasha la mkoa lenye ladha ya kimataifa.

Mashabiki walijaa uwanjani kama “Anfield ya Iringa,” huku midundo ya singeli na hip hop ikitawala anga na kugeuza uwanja wa Mlandege kuwa jukwaa la burudani.

“Mpira ni burudani, afya na ajira,” alitangaza kwa bashasha Meya wa Manispaa ya Iringa anayemaliza muda wake Ibrahim Ngwada wakati akikabidhi zawadi.

Ngwada, alikuwa mgeni rasmi, akiambatana na mgombea ubunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga, ambaye aliahidi kuwaalika mabingwa wa Mgera FC bungeni endapo atachaguliwa.

Kwa miaka mingi, mashindano ya soka mkoani Iringa yamekuwa yakijulikana kwa zawadi ndogo—mbuzi, mpira au seti ya jezi.

Vunjabei Cup inayoratibiwa na mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo ( CCM) imevunja mwiko kwa kutoa zawadi ya Sh milioni 10, ikiwasha moto wa ushindani na kuongeza thamani ya mashindano ya soka la ngazi za chini.

Mashindano hayo yalianza rasmi mapema mwaka huu yakihusisha timu 140 kutoka wilaya zote za mkoa wa Iringa, zikicheza soka la ushindani wa hali ya juu.

Na sasa, kwa Mgera FC kuinua kombe katika uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege, Iringa imepata kumbukumbu mpya: ushindi unaoweza kuamsha tena ari ya soka mkoani na, pengine, kufufua matumaini kwa timu kongwe kama Lipuli FC, iliyoangukia daraja la nne.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button