LIGI KUU BARA: Mwendo mdogo mdogo, watafika tu

LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea kushika kasi, huku baadhi ya timu zikiwa tayari zimecheza raundi tatu, mbili na zingine moja.

Kiujumla, ligi inazidi kushika kasi na kila timu ikijitahidi kujikusanyia pointi mapema, ili kufanya biashara mapema na mwishoni ibaki na kibarua cha kuhesabu faida tu, wakati huo kazi ikiwa ngumu.

Timu ya Fountain Gate ya Babati mkoani Manyara, msimu uliopita nusura ishuke daraja kama sio kuponea kwa kucheza mtoano dhidi ya Timu ya Championship ya Stand United ya Shinyanga. Fountain Gate ilipata ushindi wa jumla wa mechi na kunusurika kushuka daraja.

Wadau wengi wa michezo, hasa soka walijua kuwa Foutain Gate msimu huu itakuwa imejifunza baada ya kutaabika sana kupambana hadi dakika za mwisho kujinusuru na kushuka daraja. Ligi ndio kwanza imeanza
lakini timu hiyo imerudia tena kufanya vibaya kwa kupoteza mechi zote tatu za mwanzo na haina pointi hata moja.

Timu hiyo baada ya kucheza mechi tatu, imefungwa zote, haijafunga bao hata moja na tayari imefungwa mabao sita. Hivyo, huenda msimu huu ikamaliza ligi vibaya. Msimu uiopita wa 2024/2025, timu hiyo ilianza vizuri ila ikaja kuvurunda duru la pili kwa kufungwa mechi nyingi na kuifanya imalize katika nafasi ya 15 lakini msimu huu imeanza vibaya, sijui mwishoni itakuwaje?

Kocha Denis Kitambi ameamua kwa hiari yake kuachia ngazi kabla timu hiyo haijamfia mikononi mwake na kuharibu jina lake kubwa na maarufu, katika fani ya ukocha. Kuna sababu nyingi zinamfanya Kitambi kuachia ngazi. Moja ni kuwa uongozi wa timu hiyo kuonekana kutokuwa makini, kwani hadi sasa kuna wachezaji hawana vibali na kuwafanya kushindwa kucheza.

Timu ya Tanzania Prisons, ambayo msimu uliopota ilinusurika kushuka daraja, msimu huu haijaanza vibaya baada ya kucheza mechi tatu na kushinda mechi moja na kufungwa mechi mbili. Ina pointi tatu na iko nafasi ya 12. Timu ya Pamba baada ya kucheza mechi tatu ina pointi mbili, baada ya kutoka sare mara mbili na kufungwa mara moja. Timu hio iko nafasi ya 15.

Huku Timu ya TRA FC ambayo msimu uliopita ilijulikana kama Tabora United, ambayo ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya tano katika msimamo wa kunusurika kidogo kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, kama ingebahatika kumaliza ya nne katika msimamo wa ligi. TRA FC ipo nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi tatu na kuwa na pointi tatu, huku Coastal Union ya Tanga ina pointi tatu baada ya kucheza mechi tatu.

Imeshinda mechi moja na kufungwa mechi mbili. Mbeya City, ambayo ilikuwa na pointi mbili imefikisha pointi tatu baada ya kutoka suluhu na Yanga na kufikisha pointi tatu. Timu hiyo imepanda daraja msimu huu na kuonesha kuwa iko vizuri katika mchakato huo.

KMC iko katika nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi tatu na kuambulia pointi tatu, Singida BS iko katika nafasi ya tisa lakini imepanda baada ya kutoka sare na TRA FC, hivyo sasa ina pointi nne.

Msimu uliopita Singida BS ilimaliza nafasi ya nne katika msimamo wa ligi na kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika Kombe la Shirikisho Afrika na imesonga mbele katika hatua ya pili baada ya kushinda mechi zake nyumbani na ugenini.

Singida BS kwa sasa ipo nafasi ya pili baada ya Simba kuifunga Namungo mabao 3-0 na kushinda mechi zake zote mbili ilizocheza hadi sasa, na kuwa na jumla ya pointi sita baada ya kushinda mechi zake zote. Mwendo wa Singida Black Stars sio mbaya baada ya nayo kushinda mechi zake na kufikisha pointi sita, lakini imepitwa na Simba kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Mtibwa Sugar, timu iliyopanda na kurudi tena Ligi Kuu imeanza vizuri ligi hiyo baada ya kuwa mabingwa wa Championship baada ya kufanya vizuri. Ina pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili na kufungwa mechi moja. Timu hiyo iliwahi kuwa bingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfulilizo, katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kushika nafasi ya nane.

Azam FC, imecheza mchezo mmoja kwa sababu inashiriki mashindano ya Afrika Kombe la Shirikisho na mchezo huo imeshinda, huku kimataifa ikishinda mchezo huo na inashika nafasi ya saba katika msimamo huo. Timu zinazoshika nafasi sita za juu ni Yanga, Simba, Namungo, Mashujaa, JKT Tanzania inayoshika nafasi ya pili na Dodoma Jiji, huku Singida BS ikiongoza msimamo ikiwa na pointi sita.

Ligi hiyo ndio kwanza inaanza lakini waswahili wana msemo usemao ‘Biashara asubuhi, jioni kuhesabu mapato’. Sasa wewe kama hatafanya biashara asubuhi jioni utahesabu nini? Hata hao Fontain Gate, ambao wameanza vibaya, wanaweza kukaa sawa na kusogea lakini nao wasikate tamaa mapema, kwani yanaweza kuwakuta ya KenGold, ambayo mwanzo wa ligi hadi mwisho walishika mkia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button