Tuwekeze kwenye soka la watoto kitaalamu

NDOTO za Taifa Stars kuwa moja kati ya timu nne zitakazopata nafasi ya kucheza mechi za mchujo kuwaniakufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico mwakani, zimekufa.
Ndoto hizo zimeota mbawa baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ Uwanja wa Amaan Compex, Unguja, Zanzibar Jumatano.
Lakini kukosekana kwa nafasi hiyo kwa Taifa Stars baadhi ya mashabiki wa soka wa Tanzania wanaamini, Kocha Mkuu wa timu hiyo Hemed Suleiman ‘Morocco’ hatoshi kwa nafasi hiyo.
Morocco aliyeongoza Taifa Stars kufuzu fainali zake za tatu za Mataifa ya Afrika zitakazoanza nchini Morocco, Desemba mwaka huu anaonekana hatoshi na kwamba mashabiki hao wanaamini Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapaswa kusaka kocha mwingine atakayeifikisha Tanzania kwenye mafanikio zaidi.
SOMA: NBC, wadau waendesha kliniki ya michezo kwa watoto
Labda pengine ni kumtoa kafara kocha huyo mzawa alieonekana kuaminiwa na TFF huku zikiwekwa kando sababu za msingi zitakazolipeleka soka la Tanzania mbele zaidi na hivyo kuwa na timu ya taifa imara.
Mara kwa mara gazeti hili limekuwa mstari wa mbele kuhubiri juu ya kutengeneza msingi mzuri wa soka la vijana kuanzia umri mdogo kabisa na si kuanzia umri wa miaka 15 ama 17 ikiaminika kwa kufanya hivyo basi Taifa Stars inaweza kupata wachezaji mahiri kwa baadaye.
Kuna kila sababu wadau wote wa soka kuiunga kwa vitendo serikali kwenye juhudi zake za kutaka kuona soka la Tanzania linapiga hatua kubwa kwa kuandaa mazingira bora kwa mchezo huu kuchezwa kwa ufanisi mkubwa.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kutengeneza miundombinu rafiki kuhakikisha mchezo huu unaopendwa zaidi duniani ikiwemo ukarabati na ujenzi wa viwanja vya kisasa, unachezwa kwa kiwango cha juu na Taifa Stars inapata mafanikio makubwa.
Umri sahihi wa kuanza kuwekeza ni miaka sita na si miaka 15 au 17 kama ambavyo wachezaji wengi wa Taifa Stars wameanza kuonekana katika umri huo.
Uwekezaji kwenye soka la watoto watakaokwenda ngazi kwa ngazi unahitaji dhamira ya dhati kwa wale wote wenye mapenzi na mchezo huu wa soka ikiwemo kuajiri walimu wajuzi wa soka la umri mdogo kutoka nchi zinazosifika kwenye kuendeleza soka la vijana kama Hispania, England, Ufaransa, Ubelgiji na nyinginezo katika bara la Ulaya.
Uwekezaji unaofanywa na serikali kwenye miundombinu ya mchezo huu karibu kila kona ya nchi unapaswa kuungwa mkono na wadau wake kwa kuanza kutengeneza kitaalamu soka la watoto ambao baadaye watakuja kucheza timu za ngazi mbalimbali za vijana na mwisho Taifa Stars.
Siku mtego huu ukiteguliwa basi Tanzania itakuwa moja ya mataifa tishio katika mchezo wa soka duniani lakini kwa kuruka hatua kama ilivyo sasa basi kila kocha wa Taifa Stars atajikuta kwenye lawama.



