Hemed aahidi kufufua michezo Kiwani

MGOMBEA wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Awamu ya Nane imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya michezo kwa kujenga viwanja vipya katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar pamoja na kufanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa New Amaan Complex na Uwanja wa Gombani Pemba.
Akizungumza na wanamichezo wa Jimbo la Kiwani, Ndugu Hemed alisema hatua hizo zina lengo la kukuza sekta ya michezo nchini na kuibua vipaji vipya miongoni mwa vijana. SOMA: Mwinyi kufanya mageuzi ya kilimo

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Jimbo la Kiwani kumpa ridhaa kuwa mwakilishi wao katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, akiahidi kwamba endapo atachaguliwa, atahakikisha anaboresha mazingira ya michezo na kufufua vuguvugu la michezo katika jimbo hilo.
Hemed aliongeza kuwa anafahamu changamoto zinazowakabili wanamichezo katika eneo hilo, na hivyo atazishughulikia kwa vitendo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo na vijana.


