Mwinyi kufanya mageuzi ya kilimo

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuinua uchumi wa wakulima na wavuvi kupitia mageuzi makubwa katika sekta za mwani, mpunga na uvuvi, ikiwemo kuongeza bei ya mwani kutoka shilingi 700 hadi 1,000 kwa kilo.
Akizungumza na wakulima wa mpunga wa Cheju, wakulima wa mwani na wavuvi katika uwanja wa Marumbi, Mkoa wa Kusini Unguja, Dk. Mwinyi alisema serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya kununua mwani wote uliopo majumbani kwa bei mpya, akisisitiza kuwa sekta hiyo ni nguzo muhimu ya uchumi wa buluu.
Alisema Zanzibar inaongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa mwani, hivyo serikali itaendelea kuboresha miundombinu, masoko na teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na kuwasaidia wakulima kunufaika zaidi na zao hilo. “Tutahakikisha tunanunua mwani wote na kujenga viwanda vya kuusindika kama tulivyofanya Pemba, ili kuongeza thamani na kipato kwa wakulima,” alisema.
Akizungumzia kilimo cha mpunga, Dk. Mwinyi aliahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya mabonde yote ya mpunga, pamoja na kuongeza idadi ya matrekta, mashine za uvunaji na pembejeo bora ili wakulima wazalishe kwa wingi na kutumia teknolojia ya kisasa. SOMA: Tabianchi Yatikisa Kilimo cha Mwani
Alisema Zanzibar bado inaagiza mchele kutoka Tanzania Bara na nje ya nchi, hivyo kuna haja ya kuhakikisha uzalishaji wa ndani unaongezeka kwa ajili ya usalama wa chakula. Aidha, Dk. Mwinyi aliahidi kuendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa wakulima na wavuvi na kuondoa urasimu katika upatikanaji wake, akisisitiza kuwa sekta hizo tatu ni msingi wa uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohammed Said Dimwa, alisema Dk. Mwinyi ni kiongozi mwenye maono ambaye ameleta mabadiliko makubwa ya maendeleo na kuwataka wananchi kumpa ridhaa tena katika uchaguzi wa Oktoba 29.
Wakulima na wavuvi walimpongeza Dk. Mwinyi kwa hatua za kuimarisha sekta zao, huku Fatma Abdalla, mkulima wa mwani, akiomba serikali kuendelea kuwapatia vifaa vya kilimo cha mwani na kuongeza bei ya zao hilo, na Ali Nassor wa Chwaka akitaka serikali ijikite zaidi kwenye uvuvi wa bahari kuu na udhibiti wa uvuvi haramu.


