Rais Samia aendeleza mapambano ya Nyerere

MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi wachache waliodhihirisha kwa vitendo namna ya kuuenzi na kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, hususan katika mapambano dhidi ya maadui watatu wa maendeleo ujinga, maradhi na umasikini.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Kindiko, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Dk. Nchimbi alisema Rais Samia ameonesha uongozi wa mfano kwa kuendeleza mapambano hayo kupitia miradi mikubwa ya elimu, afya na uchumi.

Akinukuu hotuba ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ya Desemba 9, 1961, Dk. Nchimbi alikumbusha kauli ya Baba wa Taifa aliyowahi kusema: “Maadui wakuu wa nchi yetu ni ujinga, maradhi na umasikini.”SOMA: Mwinyi atangaza mkakati mpya sekta ya afya
Alisema kauli hiyo bado ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya taifa, na kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Samia inaendelea kupambana na maadui hao kwa nguvu zote.
“Rais Samia amekuwa kiongozi anayeendeleza mapambano haya kwa vitendo. Amejielekeza kuimarisha sekta ya elimu, kuboresha huduma za afya na kukuza uchumi wa taifa letu. Ni kiongozi anayetekeleza kwa vitendo dira ya Mwalimu Nyerere,” alisema Dk. Nchimbi.

Aliongeza kuwa uongozi wa Rais Samia umeendelea kuimarisha umoja wa kitaifa, ustawi wa wananchi na kuendeleza misingi ya maendeleo iliyowekwa tangu enzi za Baba wa Taifa.


