Ruto aitisha kikao kufuatia msiba wa kitaifa

RAIS wa Kenya, William Ruto, leo ameingia katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Kitaifa, huku akitarajiwa kuongoza pia kikao maalum cha Baraza la Mawaziri kufuatia msiba wa kitaifa wa kiongozi wa kisiasa na Waziri Mkuu Mstafu, Raila Odinga.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula, ameahirisha kikao cha Bunge kufuatia msiba huu. Hatua hiyo inatoa nafasi kwa viongozi wa taifa hilo kushughulikia taratibu za heshima na mipango ya kitaifa. SOMA: Ruto, Museveni wamuunga mkono Odinga

Rais Ruto anatarajiwa kuhutubia taifa leo. Hotuba yake itahusu: kifo cha Raila Odinga, heshima za kitaifa, na hatua zinazofuata kuhakikisha usalama, utulivu na mshikamano wa taifa. “Rais Ruto anataka kuhakikisha taifa linashughulikia msiba huu kwa heshima na mshikamano,” taarifa ilisema.

Raila Odinga alifariki akiwa nchini India wakati akipatiwa matibabu maalum. Odinga alikuwa mgombea wa urais mara kadhaa na kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Kenya, aliyechangia pakubwa katika maendeleo ya kidemokrasia na siasa za taifa.

Viongozi wa serikali na wananchi wameeleza huzuni yao kupitia mitandao na vyombo vya habari. Msemaji wa chama cha ODM alisema: “Kenya imepoteza kiongozi shupavu wa siasa za kidemokrasia. Mchango wake utaendelea kuishi katika historia ya taifa letu.”

Kifo cha Odinga kimeibua mjadala kuhusu mustakabali wa siasa za upinzani nchini Kenya. Viongozi wa vyama vya kisiasa wametoa wito wa mshikamano na heshima za kitaifa, huku wananchi wakiendelea kuomboleza kufuatia msiba huo.

Katika taarifa  aliyotoa Rais  Ruto alisema:“Tunapaswa kuungana kama taifa katika msiba huu na kuheshimu mchango wa Raila Odinga katika siasa za Kenya.” Kwa sasa, taifa la Kenya linasubiri hotuba ya Rais Ruto itakayotoa mwongozo wa hatua zinazofuata. Wananchi wanatarajia  kutoa heshima za kitaifa pale itakapotangazwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button