Ngajilo aahidi timu ligi kuu

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, ameahidi kuwa moja ya vipaumbele vyake katika kipindi cha miaka mitano ya ubunge wake ni kuhakikisha mkoa wa Iringa unapata tena timu ya kucheza Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara (NBC Premier League).

Akizungumza katika mikutano yake ya kampeni katika kata mbalimbali za jimbo hilo, Ngajilo alisema ni jambo la kusikitisha kuona mkoa wenye historia na vipaji vikubwa kama Iringa unakosa timu ya ligi kuu, licha ya juhudi nyingi zilizowahi kufanyika huko nyuma.

“Iringa inastahili kuwa na timu ya ligi kuu. Katika miaka mitano ya ubunge wangu, nitahakikisha tunarudisha heshima hiyo kwa kuunda mfumo imara wa kuikuza timu ya mkoa wetu. Timu hiyo itakuwa chachu ya michezo na ajira kwa vijana,” alisema Ngajilo.

Ngajilo alikumbusha kuwa Iringa iliwahi kuwa na fahari kubwa kupitia Lipuli FC, timu ambayo kwa miaka mingi ilibeba matumaini ya wakazi wa mkoa huo.

Lipuli FC ilipanda daraja na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1990, kabla ya kushuka tena kutokana na changamoto za kifedha na kiutawala.

Baada ya miaka mingi ya kusota, timu hiyo ilifanikiwa kurejea Ligi Kuu msimu wa 2017/2018, ikicheza michezo mikali dhidi ya timu kongwe kama Yanga, Simba na Azam.

Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa udhamini na matatizo ya uongozi, Lipuli FC ilishuka tena daraja mwishoni mwa msimu wa 2020/2021, ikiweka majonzi makubwa kwa mashabiki wake.

Baada ya kuanguka kwa Lipuli, wadau wa soka mkoani Iringa hawakukata tamaa. Kwa nguvu zao, walifanikiwa kununua timu ya Ruvu Shooting, iliyokuwa ikicheza Ligi Daraja la Kwanza, wakilenga kuirejesha hadi Ligi Kuu kwa jina jipya na nguvu mpya.

Hata hivyo, ndoto hiyo haikudumu. Licha ya jitihada kubwa, timu hiyo nayo ilishuka daraja msimu wa 2023/2024, na kuacha matumaini ya mashabiki wa Iringa yakiwa yameyeyuka tena.

Licha ya changamoto hizo, Ngajilo amekuwa mmoja wa wadau waliodumu kuwekeza katika michezo kupitia mashindano ya Ngajilo Cup, ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika jimbo la Iringa Mjini.

Mashindano hayo yanashirikisha timu kutoka kata mbalimbali za mkoa wa Iringa, yakiwa na lengo la kukuza vipaji vya vijana na kuwaunganisha wakazi wa Iringa kupitia michezo.

“Ngajilo Cup imekuwa jukwaa la vijana kuonesha uwezo wao. Wengi wamepata nafasi ya kucheza katika timu kubwa kupitia mashindano haya, na naamini tukiunganisha nguvu hii, tutaunda timu ya ligi kuu kutoka Iringa,” alisema.

Mashindano ya Ngajilo Cup yamejizolea umaarufu kutokana na hamasa kubwa ya wananchi, zawadi nono (mshindi wa kwanza Sh Milioni 10), na nidhamu inayosimamiwa kwa viwango vya kitaalamu.

Kwa sasa, yanatajwa kuwa moja ya mashindano ya kijamii yenye ushawishi mkubwa mkoani Iringa.

Ngajilo amesema endapo atapata nafasi ya kuwa mbunge, atashirikiana na wadau wa michezo, wafanyabiashara, na halmashauri kuanzisha timu mpya itakayokuwa mfano wa kitaifa kwa usimamizi na uwekezaji.

“Jina la timu hiyo ni kitendawili kwa sasa,” alisema huku akicheka, “haiwezi kuwa Lipuli wala Ruvu Shooting. Tunataka kuanza upya, na kuijenga timu itakayodumu na kuwakilisha Iringa kwa fahari.”

Ameongeza kuwa mradi huo wa michezo utaenda sambamba na kuinua viwanja vya michezo, kuanzisha ligi za mitaani, na programu za kukuza vijana wenye vipaji.

Kwa mashabiki wa soka Iringa, ahadi hii ya Ngajilo imeamsha kumbukumbu, matumaini na mijadala mikali mitaani kuhusu hatma ya soka la mkoa huo.

Wengi wanasema, kama atafanikiwa kutimiza ahadi hiyo, basi itakuwa historia mpya kwa michezo ya Iringa.

Habari Zifananazo

9 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button