Kimiti: Vijana wasikilizwe, wawe suluhu

JAMII imehimizwa kujenga utamaduni wa kusikiliza vijana ili wajihisi ni sehemu ya viongozi katika kuchangia uamuzi kuhusu maendeleo ya nchi yao. Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere (MNF), Paul Kimiti alisema vijana wakisikilizwa mawazo yao na wakasema wanachohitaji watajiamini ndani ya familia zao na taifa kwa ujumla. “Tunapaswa kwa kweli kuandaa mazingira mazuri ambayo yatawafanya vijana kujiona ni sehemu muhimu ya viongozi ndani ya familia, jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Kimiti alipozungumza na HabariLEO.
Alisema kupitia mfumo huo vijana watajitambua vizuri na watakuwa na uelewa wa mambo mengi hivyo kuwa vigumu kuchotwa na mihemko ambayo mwisho wake wanaishia kujuta hata kupoteza mwelekeo.
Aidha, Kimiti anaeleza kuwa kijana bora katika nchi anapaswa kuandaliwa kiuongozi na wazazi na jamii husika.
Alisema malezi bora ni muhimu zaidi kwani watoto hujengwa na miiko ya uongozi ya wazazi wao.
“Changamoto ni kwamba tumewaacha watoto wafanye wanavyotaka jambo ambalo si sawa, hiyo si demokrasia. Wazee wanapaswa kutekeleza jukumu lao la uzazi kama msingi wa malezi bora ya watoto wao,” aliongeza Kimiti.
Akisimulia safari yake kuanzia akiwa kijana hadi sasa, anasema kisiasa ilikuwa nzuri na ya kupigiwa mfano, ikiwa ni urithi wa uongozi bora aliopata kutoka kwa baba yake, Peter Kimiti ambaye alikuwa dereva wa teksi enzi za ukoloni. “Nakumbuka mwaka 1954 wakati wa utawala wa Uingereza, baba yangu alitunukiwa nishani na Malkia Elizabeth kwa kutambua utendaji kazi wake bora kama dereva anayetoa huduma kwa umma,” aliongeza Kimiti.
Kimiti alisema mafanikio hayo ya kitaaluma yamechagiza uongozi wake na kuwa ukumbusho wa kudumu wa thamani ya kuheshimu kazi na kuifanya kwa bidii. Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, katika maisha yake ya kisiasa mwaka 1987, alitunukiwa nishani na Rais Ali Hassan Mwinyi kutokana na utendaji wake wa kuigwa akiwa mkuu wa mkoa.
Alitoa wito itolewe elimu ya uraia kwa vijana kuhusu umuhimu wa kuwa wazalendo, kuchangia maendeleo ya taifa na kupenda nchi yao ili kuwa na vijana wanaolipenda taifa lao. Alisisitiza kuwa lazima vijana wajue kuwa kiongozi mzuri ni anayesuluhisha shida za watu, anayesimamia haki na kutoa huduma kwa watu wote bila upendeleo.SOMA: Kimiti: Hakuna aliyefanikiwa kwa vurugu
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema jukumu la kujenga vijana waadilifu na wanaothamini taifa lao ni kuanzia kwa wazazi. Alisema vijana wanatakiwa kufundishwa utaifa kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora ni nguzo nne za maendeleo ya nchi.
Kuhusu vijana na siasa, Dk Mbunda aliishauri serikali kuendelea kuhakikisha chaguzi zote zinatabirika kwa kuwa huru na haki ili kuwa na uhalali wa kisiasa kwa watu wote, wakiwemo vijana kujihusisha na siasa kwa amani na kuthamini mamlaka ya wao kupigiwa kura au kuchagua viongozi wanaowapenda.Dk Mbunda alisema vijana ambao ni sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini wana uwezo wa kushawishi uchaguzi kwa kuzingatia uwezo wao wa kuhama na kubadilika kulingana na upepo wa kisiasa unavyovuma wakati husika.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema vijana wengi hawajui maana halisi ya siasa za upinzani wakidhani ni kuwa adui kisiasa. Alisema kutokana na dhana hiyo, ndiyo maana ni rahisi Tanzania ya sasa vijana kuchotwa kiakili na mtu yeyote atakayeamua kwenda kinyume na serikali kwa sababu wanajua serikali adui yake ni upinzani.
“Serikali ijenge mazingira kwa kuandaa jukwaa la vijana ambalo ndani yake, taasisi, mashirika na watu binafsi wanaweza kuingia na kutoa elimu ya uongozi kwa vijana ili watambue na kutofautisha siasa za upinzani kwa hoja na mihemko,” alishauri Massawe.
Aliwataka vijana wanaotaka mageuzi serikalini au katika taasisi za serikali huku wakikimbia majukwaa rasmi na halali ya kupeleka madai yao, kubadili mbinu hiyo ya kizamani, badala yake wahakikishe wanadai mambo yao wakiwa katika mfumo rasmi ili iwe rahisi kueleweka. Kwa upande wake, Mbunge mteule kundi la vijana Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zainab Abdallah Issa alisema chama kingependa vijana wote bila kujali itikadi, wawe kitu kimoja katika kujenga taifa lao kwa sababu vijana ndio taifa la leo na baadaye.
Sambamba na hilo, Zainabu alisema kuwa serikali haina mtoto wa mgongoni na wa tumboni, kwa maana ya vijana wa chama tawala na wa upinzani bali wote ni wake, ndio maana fursa zinazoletwa haziji kwa majina ya vijana wa CCM bali zinakuja kwa majina ya vijana wote nchini. “Kuna sera ya kujenga viwanda nchi nzima na hivi zaidi ya asilimia 90 vinakwenda kuajiri vijana na zaidi ya asilimia 90 ya vijana ndio watengenezaji wa miundombinu ya vijana,” alisema Zainabu.
Alisema akiwa kiongozi wa vijana anawasihi vijana kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na namna anavyowajali vijana na kuwapa kipaumbele. “Nawaasa vijana wasikubali kurubuniwa kwa namna yoyote ile, wasikubali kudanganywa kujiingiza kwenye maandamano wakati wanaoongoza maandamano hayo hawapo nchini, wako nje ya nchi wanaishi maisha mazuri raha mustarehe. Anakushawishi uandamane, ukija kuvunjwa mguu wanaohangaika ni familia yako, yeye anaendelea na maisha yake,” alisisitiza Zainabu.
Alisema serikali kwa kuwathamini vijana imewaamini na kuwapa nafasi kubwa za maamuzi. Alitolea mfano kwa baraza la mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya nafasi zote za uteuzi zaidi ya asilimia 90 ni vijana, ikiwa ni ahadi ya Rais Samia kuwa Watanzania watarajie watakaoteuliwa wengi watakuwa vijana, kwa sababu leo na kesho ya taifa letu ni vijana. Alisema vijana wanamshukuru Samia kwa kuwaamini na kuwapa nafasi za uongozi kimaamuzi, kwa hiyo lazima wamuoneshe wanamuunga mkono.