Kimiti: Hakuna aliyefanikiwa kwa vurugu

MWENYEKITI wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, ambaye pia amepata kuwa waziri kwenye wizara mbalimbali nchini,  Paul Kimiti, ameomba Watanzania kuendelea kuenzi na kudumisha urithi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, hasa katika kulinda amani na mshikamano wa taifa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Daily News Digital jijini Dar es Salaam, Kimiti amesema Tanzania itaendelea kuwa imara endapo kizazi cha sasa, hususan vijana, kitathamini na kufahamu kuwa nchi ni yao na wanawajibika kuilinda kwa moyo wa uzalendo kama alivyosisitiza Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.

“Wananchi wetu wajue majukumu yao wanaposikia sera mbalimbali. Hata kama hukubaliani na sera hizo , si suala la kulalama au kupiga kelele. Hilo si suluhisho. “ Ukikubali au hukubali, uamuzi wako una nafasi yake kwenye kura. Mwalimu alitufundisha kuheshimu demokrasia na maamuzi ya wengi, na kufanya fujo hakusaidii kitu chochote,” amesema Kimiti.

Amesema misingi hiyo ya amani, umoja na mazungumzo badala ya vurugu ndiyo siri kubwa iliyoliwezesha taifa la Tanzania kubaki kuwa kisiwa cha amanii Afrika kwa zaidi ya nusu karne tangu kupata uhuru. “Vijana wakitaka wafanikiwe katika maisha yao lazima waelewe nchi ni yao, lazima waipende na wailee. Tukifika mahali ambapo hatuoni umuhimu wa amani, tunajiharibia wenyewe. Hakuna aliyewahi kufanikiwa kupitia vurugu. Wengi wamekosa amani kwa sababu ya kuacha misingi aliyoasisi Mwalimu Nyerere,” ameongeza Kimiti.

Kuenzi alama ya Mwalimu Nyerere

Kauli ya Kimiti imekuja wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 26 tangu kufariki dunia kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14, 1999. Katika kipindi chote hicho, Watanzania wameendelea kuenzi mchango wake katika kujenga taifa lenye umoja, amani, usawa na kujitegemea.

Mwalimu Nyerere, kupitia sera yake ya Ujamaa na Kujitegemea, alihimiza wananchi kuwa wamoja na kufanya kazi kwa bidii ili taifa lijitegemee kiuchumi. Alikuwa kiongozi wa mfano, aliyesisitiza maadili, uadilifu na upendo kwa taifa lake. SOMA: Waandishi Bunifu waalikwa kushiriki Tuzo ya Mwalimu Nyerere

Urithi unaodumu vizazi kwa vizazi

Kwa mujibu wa Kimiti, taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere itaendelea kuelimisha vijana kuhusu falsafa na misingi aliyoacha Baba wa Taifa, ili kizazi kipya kijifunze maadili ya uzalendo, uwajibikaji na kuheshimu misingi ya kidemokrasia. “Mwalimu alitupa dira. Ni wajibu wetu kuilinda amani hii kwa vitendo, si kwa maneno. Vijana ndio tegemeo la taifa, wakipotea kwenye vurugu, taifa zima linayumba,” amesema.

Kwa hakika, Mwalimu Nyerere aliweka alama isiyofutika katika historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla alama ya upendo, umoja na amani. Kama alivyoeleza Mwalimu mwenyewe: “Amani haiji kwa bahati, bali ni matokeo ya haki na kuheshimiana.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button