Uaminifu na nidhamu iwe nguzo ya vijana vyuoni

KILA mwaka maelfu ya vijana nchini huanza safari mpya ya kielimu katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali. Ni hatua ya fahari kwao na kwa familia zao, kwani chuo ni lango la mafanikio na maendeleo binafsi.
Hata hivyo changamoto kubwa imekuwa ni baadhi ya vijana kutumia vibaya uhuru wa maisha ya chuo na kujihusisha na vitendo viovu vinavyohatarisha ndoto zao.
Siku chache zilizopita Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilitangaza kukamata watuhu- miwa wanne waliodaiwa kutengeneza biskuti za bangi kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
SOMA: NEDC yatafsiri Dira 2050 maendeleo kwa vijana
Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo baadhi ya watuhumiwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu, wengine wakiwa walifeli masomo wakiwa mwaka wa pili na wengine wamehitimu.
Taarifa hii inasikitisha hasa kuona kuwa baadhi ya vijana wanapofika vyuoni wanasahau kilichowapeleka na kusombwa na wimbi la makundi ya waovu.
Ni ukweli usiopingika kuwa vyuo ni mahali pa kupata elimu ya juu, ujuzi na maarifa yatakayojenga taifa la kesho, lakini kwa wengine, vyuo vimekuwa uwanja wa ulevi, anasa, uvivu wa masomo, uasherati na matumizi ya dawa za kulevya.
Matokeo yake ni wanafunzi kupoteza mwelekeo, kuacha masomo au hata kuingia katika matatizo ya kisheria na kiafya na udhihirisho ni taarifa ya DCEA iliyobainisha namna vijana wanaojiunga vyuoni na kujihusisha na vitendo vya kihalifu kama kutengeneza biskuti zenye dawa za kulevya na kuziuza vyuoni na wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kuandaa na kufanya sherehe zinazohusisha matendo yanayokwenda kinyume na maadili kwa madai ya kukaribisha wanafunzi mwaka wa kwanza.
Vijana wanapaswa kutambua kwamba maisha ya chuo yanahitaji nidhamu ya hali ya juu. Uhuru walioupata haupaswi kutumiwa vibaya, bali uwe fursa ya kujifunza kujisimamia.
Tunaamini mwanafunzi mwenye maadili na malengo thabiti ataweka vipaumbele vyake katika masomo, kujijenga kielimu na kimaadili na kuepuka vishawishi vya marafiki wabaya.
Kuna haja pia ya taasisi za elimu na jamii kwa jumla kuimarisha malezi ya kimaadili kwa watoto kwani wanatokea mikononi mwa wazazi na walezi kabla ya kujiunga vyuoni kama wanafunzi.
Elimu bila maadili ni kama taa isiyokuwa na mwanga. Vyuo viweke programu za ushauri, semina za maadili na hata klabu za vijana zitakazowasaidia wanafunzi kuelewa thamani ya maisha yenye nidhamu na uwajibikaji.
Taifa linatarajia vijana wenye maadili, walioelimika na wenye maono, hivyo jamii ibebe jukumu lake kwa kuchukua hatua ya kuwalea vijana na kuwasihi watumie fursa ya elimu wanayopata kujenga maisha yao na kuepuka vitendo vitaka- vyowaangamiza na kuzima ndoto zao.




Freedom to work whenever I want — that’s what I love! I made $18,542 in a month doing this online. Check the details ———————⊃⫸ https://dailycash21.blogspot.com/