Vifaa vya uchaguzi vyawasili Arusha

ARUSHA: MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vimeshawasili mkoani Arusha kwa ajili ya kusambazwa katika jumla ya vituo vya kupigia kura 1,051 vyenye idadi ya wapigakura 435,119 kwa jiji la Arusha
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha, DC Joseph Mkude amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwani ulinzi na usalama umeimarishwa huku akisisitiza hakuna maandamano Oktoba 29 bali wananchi watimize wajibu wao wa kupiga kura.
Amesema vifaa hivyo vya uchaguzi vitasambazwa kwenye mitaa 154 iliyopo jiji la Arusha huku akiongeza kuwa kampeni katika vyama mbalimbali zilifanyika kwa maeneo mbalimbali ikiwemo vyama vingine kuhitimisha kampeni zao leo kesho.

“Kampeni kwa jiji la Arusha zimeenda vizuri na hakuna fujo yoyote ile iliyotokea wagombea udiwani na ubunge walinadi sera zao vizuri na wengine wanafunga kampeni zao leo(kesho jumatano) huku ulinzi na usalama ukiwa umeimarishwa” amesema.

Amesisitiza kuwa wananchi wajitokeze kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu na kuwatoa hofu kuwa hakuna maandamano yoyote yatakayotokea bali kazi kubwa ni kupiga kura na kwenda nyumbani.



