Mgombea urais Makini aahidi pareto Kilimanjaro

KILIMANJARO; MGOMBEA urais kupitia Chama cha Makini, Coaster Kibonde amesema serikali ya chama hicho itaanzisha kilimo cha pareto Mkoa wa Kilimanjaro ili kuimarisha uchumi wa mkoa huo.
Kibonde alisema hayo wakati wa mkutano wa kampeni katika viwanja vya soko la Manyema, Manispaa ya Moshi mkoani humo juzi.
“Utafiti uliofanywa na wataalamu wa chama chetu umebaini kuwa zao la pareto ambalo nalo ni muhimu katika kukuza uchumi kutokana na kuwa na soko kubwa maeneo mbalimbali duniani kote linaweza kustawi mkoani Kilimanjaro,” alisema.
Aliongeza: “Kahawa ndiyo lilikuwa zao muhimu kiuchumi lakini kwa sasa limeshuka kutokana na sababu mbalimbali, njia ya kuimarisha uchumi wenu na wa mkoa kwa ujumla ni kuanzisha kilimo cha zao lingine”.
Akizungumzia zaidi kuhusu kilimo, Kibonde alisema serikali yake itaboresha viwanja vya ndege katika mikoa yote ili kurahisisha mauzo ya mazao yanayozalishwa nchini.
“Viwanja hivi vikiwa bora, wakulima watakuwa na uwezo wa kusafirisha mazao yao kwa urahisi badala ya kutegemea uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere-JNIA) na ule wa KIA (Kilimanjaro International Airport)” alisema Kibonde.
Aliongeza: “Kuna wafanyabiashara wa nje ambao wanapenda kuja kununua mazao moja kwa moja hapa nchini, hawa nao watanufaika maana watakuwa wanashukia kwenye uwanja ulioko eneo analokwenda kununua mazao ya kilimo badala ya kushukia Kilimanjaro au Dar es Salaam na kisha kuanza safari ya kwenda maeneo yaliko mazao anayotaka kununua.”
Kwa upande wa elimu, Kibonde alisema serikali ya Makini itaanzisha mpango wa kugharimia elimu ya juu kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi.
“Serikali itakayoongozwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Makini itahakikisha inagharamia wanafunzi wote wanaokwenda kusoma nje ya nchi; haitakuwa ni mikopo kwao bali ni kwa ajili yao ili wapate elimu nzuri waje kuliongoza taifa baadaye”, alisema.
Kibonde pia alisema katika sekta hiyo ya elimu, baada ya kuapishwa kuwa rais atapandisha mishahara ya walimu.
“Hawa ndio watu muhimu kabisa katika taifa letu maana hakuna aliyefika hapa tulipo sasa hivi kila mtu na fani yake ambaye hakupitia kwa Mwalimu,” alisema.



