‘Arusha ni njema atakaye na aje’

ARUSHA; Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewahakikishia wananchi mkoani humo, wageni na watalii wanaofika Arusha kuwa hali ya ulinzi na usalama ni shwari na shughuli za kijamii na kiuchumi zimerejea katika hali yake ya kawaida.
Makalla amebainisha hayo leo Jumanne Novemba 04, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, akisema kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga pia kuhakikisha huduma za ulinzi na usalama zinakuwepo muda wote, ili kuruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi kuendelea kama ilivyo kawaida.

Pia katika kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hapo jana, CPA Makalla amewataka wamiliki wa vituo vya mafuta kufungua vituo vyao pamoja na maeneo mengine ya biashara, akiwataka viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kuendelea kutimiza jukumu lao la kuhakikisha usalama unakuwepo wa kutosha katika maeneo yao na kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria kwa mamlaka husika.



