Manufaa lukuki utafiti wa mafuta, gesi Bonde la Eyasi Wembere

“TUMELETA vifaa vya kisasa na vya kutosha zikiwemo mashine zaidi ya 20 za kuchimba kwenye maji na tumeongeza wataalamu kutoka Ulaya na nchi nyingine za Afrika ili kupata taarifa nzuri zaidi na zenye tija zitakazosaidia upatikanaji wa mafuta.”

Anasema Mwenyekiti wa kampuni ya Africa Geophysical Services (AGS) ambayo ni mkandarasi anayesimamia utafiti wa mafuta na gesi katika Bonde la Eyasi Wembere, Salim Haji na kusisitiza kuwa, wanatambua umuhimu wa mradi huo kwa kwa taifa, hivyo watahakikisha utafiti unakamilika Aprili mwakani kama serikali ilivyoagiza.

Katika ziara ya hivi karibuni wilayani Karatu mkoani Arusha ambako mradi huo unatekelezwa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio anabainisha kuwa, mradi huo wa kimkakati wa serikali wa utafiti wa mafuta na gesi ulioanza mwaka 2015 ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa.

Anasema hadi sasa mradi unaonesha viashiria na matumaini makubwa ya kupatikana kwa mafuta na gesi katika eneo hilo la Eyasi Wembere ambalo liko katika Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.

“Awamu ya pili ya utafiti wa uchukuaji wa taarifa za mitetemo imekamilika kwa asilimia 47 na taarifa za mitetemo zimeshachukuliwa katika eneo lenye ukubwa wa kilometa 430 kati ya kilometa 914. Utafiti huu mpaka kukamilika utaigharimu serikali Shilingi bilioni 43,” anasema Mataragio.

Anasisitiza: “Japo kazi inaendelea vizuri, tunamuomba mkandarasi, aongeze kasi, tunataka utafiti huu ukamilike ifikapo Aprili mwakani (2026) ili hatua nyingine za mradi ianze.”

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo wa wizara, mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kutekelezwa na Watanzania kwa asilimia 90 na hivyo, kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka mradi takribani 500 tangu ulipoanza mwaka 2015.

Aidha, faida nyingine ya mradi huo wa utafiti ni kurejesha fadhila kwa jamii (CSR) ambapo kuna mabwawa na visima vya maji yamechimbwa kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa eneo hilo pamoja na kuchangia huduma ya elimu na michezo.

Faida nyingine kwa mujibu wa Dk Mataragio ni pamoja na nchi kupata kiasi kikubwa cha mafuta na gesi na hivyo, kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza nishati hiyo. Anasema manufaa mengine ni uwezekano wa kupatikana kwa mafuta katika eneo hilo kwa kuwa tayari nchi za Uganda na Kenya ambazo nazo zipo katika Bonde la Ufa la Afrika Mashariki tayari zimeshagundua mafuta.

Kwa msingi huo, Dk Mataragio anaamini katika Bonde la Eyasi Wembere nako mafuta yanaweza kupatikana kutokana na viashiria vilivyoanza kuonekana. “Taarifa zinazopatikana hapa kwa njia ya mitetemo pia zinatumika na sekta nyingine kama maji na madini,” anasema Dk Mataragio.

Anaongeza: “Tayari kuna kampuni ambazo zimeshanunua taarifa zinazotokana na utafiti huu na Shirika la Maendeleo la Petroli la Taifa (TPDC) ambao ni wasimamizi wa mradi huu tayari wameshaingiza Shilingi bilioni 4.5 kwa kuuza taarifa hizo.”

Katika hatua nyingine anasema kazi kwa njia ya mitetemo inalenga kuangalia kwa kina miamba yenye kuhifadhi mafuta na kutafuta sehemu ya kuchoronga visima virefu.

Anafahamisha kuwa, taarifa za awali za utafiti zilizoanza 2015 kwa njia ya ndege na uchorongaji visima vifupi ziligharimu takribani Shilingi bilioni nane na kwamba, taarifa za awamu ya kwanza kwa njia ya mitetemo yenye urefu wa kilometa 260 ziligharimu takribani Sh bilioni 10.

Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji Mafuta na Gesi wa TPDC, Paschal Njiko anasema TPDC inafanya utafiti katika bonde hilo kwa kushirikiana na mkandarasi mzawa ambaye ni kampuni ya AGS. Kwa mujibu wa Njiko, AGS itatekeleza maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia Naibu Katibu Mkuu, Mataragio kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati.

Meneja Mkuu wa AGS, Shaum Graham anaishukuru serikali kupitia TPDC kwa kuiamini kampuni hiyo na kufanya nao kazi kwa kuwa AGS inazingatia weledi, utaalamu na matumizi ya teknolojia za kisasa. Wafanyakazi wazawa
akiwemo Pastory Maduka na Kubilu Kumalija wanashukuru serikali na AGS kwa utekelezaji wa mradi huo ambao umewapatia ajira na ujuzi kuhusu utafiti wa mafuta na gesi.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Nowadays earning money online is very easy . Eanrs every month online more than $17k by doing very easy home based job in part time u can also do this simple online Job by visiting websiteMore Details For Us→→ http://www.job40.media

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button