Mikono ya vijana ‘ijenge nyumba’ yao si kuibomoa
WADAU mbalimbali wa maendeleo kwa nyakati tofauti wanazungumzia nafasi na umuhimu wa nguvukazi ya vijana kujenga nyumba yao (taifa), badala ya kuibomoa.
Katika mazungumzo na gazeti la HabariLEO kwa nyakati na mazingira tofauti, wanasema madhara ya namna yoyote ya kutowajibika kutetea, kulinda na kuendeleza jamii na taifa kwa ujumla, huonekana katika kuangamiza familia yake ambayo ni baba, mama, watoto, ndugu, jamaa na marafiki.
Kwa nafasi na nyakati tofauti, wadau hao wanataka vijana kuwa chanzo cha amani na utulivu badala ya kuwa fimbo ya kuangamiza taifa kwa kuharibu mali ya umma. Wanasema kufanya hivyo, husababisha madhara na hasara mbalimbali ikiwamo ya upotevu wa nguvu kazi ya taifa bila sababu hali ambayo madhara yake, huwarudia wenyewe kama iwavyo kwa mpiga ngumi ukuta ambaye huumiza mkono wake.
Wanahimiza vijana kuwa makini na kuepuka kutumiwa na watu, makundi au taasisi mbalimbali zenye maslahi binafsi bila kujali maslahi na watu. Wanahimiza vijana kuungana na serikali katika jitihada za kujenga taifa moja linaloenzi tunu za taifa kama amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.
SOMA: Uaminifu na nidhamu iwe nguzo ya vijana vyuoni
Wanajikita katika ushiriki wa vijana kujenga taifa kwa kutumia siasa za hoja zinazolenga kujenga taifa na watu wake, badala ya kurubuniwa hadi kutumiwa na watu wasiotaka Tanzania iwe na amani.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Edward Mpogolo anahimiza vijana watambue nafasi zao ili wawe suluhu ya matatizo na changamoto za nchi kwamba, katu wasikubali kuwa chanzo, sababu wala mchango wa mateso kwa jamii.
Kwamba, vijana wawe walinzi na watetezi wa amani, usalama na mshikamano wa kitaifa huku wakishirikiana na jamii kutengeneza fursa zitakazokuwa chanzo cha manufaa kwao na kwa taifa badala ya kutumia mikono yao kuangamiza taifa. Kwa mujibu wa Mpogolo, vijana wawe chimbuko la amani na utulivu kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Kwanza kabisa, kama vijana tuna jukumu la kuendeleza amani kwa sababu taifa linatutegemea sisi,” anasema Mpogolo na kusisitiza kuwa amani ni msingi wa haki. Anawataka vijana kuwa kitu kimoja na kusimama pamoja na serikali yao kujenga taifa lenye mwelekeo mmoja huku wananchi wakiwa wamoja kama taifa.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Historia ya Tanzania katika Harakati za Ukombozi, Mohamed Said anawataka Watanzania kusimama kidete kupinga vitendo vya kihuni vikiwamo vinavyolenga kuharibu amani na taswira ya nchi.
Said anasema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alionya mapema Watanzania wasiangalie kwingine kisha wakafanya kosa la kujishangaa kuwa mbona wao hawapigani.
Anawataka Watanzania kuzingatia kuwa, popote duniani vurugu zinapoanza na kukosekana amani na utulivu, madhara yake hayabagui wala kupendelea, badala yake huwakumba waliomo na wasiokuwa hivyo, wengine wakiwamo wa mataifa jirani wawe kioo cha kujitazamia na kujisahihisha.
Kuhusu suala hilo, wadau mbalimbali wanasema ni pamoja na kukosa fursa za uzalishaji mali na kipato, kukosa na kudorora kwa huduma za kijamii zikiwamo za afya na kukosa masoko ya mahitaji mbalimbali.
Said anasema: “Ndicho kilichotokea katika siku tano za vurugu kuanzia siku ya uchaguzi ambapo hata waliokuwa nyumbani waliathirika kwa namna mbalimbali ikiwamo kushindwa kwenda dukani kununua mahitaji kwani hata maduka mengi hayakutoa huduma.”
Anataka vijana kujenga utamaduni si wa kutazama mbele, bali hasa kuangalia mbali ili kubaini mapema mambo yanayoweza kutokea na kuathiri vibaya mustakabali wa taifa lao.
Anataka vijana kuzingatia kuwa, kwa kutumia vurugu kamwe hawawezi kushinda au kufikia malengo yao, badala yake watapoteza maisha na kuambulia madhara mbalimbali yakiwamo ya ulemavu wa kudumu na kuzidi kujitumbukiza katika tope la umaskini, badala ya walichotaka.
“Nawapa vijana wetu mfano mzuri, vijana wenzao wa Kenya vurugu zilipamba moto na dunia nzima wakaona, lakini leo tutazame ile hasara waliyopata; waliambulia nini cha maana, wamepata lipi la maana!” anasema. Kwa mujibu wa Said, ili kudhibiti hali hiyo na kuituliza serikali iendeleze wajibu wake kusilikiza wananchi mapema na iendeleze utamaduni wa mazungumzo.
Anasema kufanya hivyo kwa kawaida huepusha uwezekano wa kutokea manung’uniko na hatimaye vurugu. Mwanasiasa Mkongwe, Paul Kimiti anasema vijana ndio nguvu kazi ya taifa. Anasema serikali inapaswa kukaa na vijana kujadili na kupanga namna ya kushughulikia mambo yao ili waone mwanga na kujenga kesho bora kwa maisha yao na taifa kwa ujumla.
Anahimiza vijana kutulia pamoja na kushirikiana ipasavyo na uongozi na serikali uliyopo madarakani kutekeleza mipango ya kuwezesha vijana iliyopo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025 hadi 2030.
“Vijana wanahitaji kuoneshwa mwanga tu wa namna ya kuyapata mafanikio, na hilo ameshalianzisha Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha katika miradi ya mashamba ya kilimo cha umwagiliaji, miradi ya vijana ya uvuvi na miradi ya kulima na kurina asali ambayo imewaajiri maelfu ya vijana na kujipatia fedha nyingi,” anasema Kimiti.
Anapongeza viongozi wa vyama vya upinzani kutokana na uthubutu wao kuhubiri amani na utulivu katika mikutano yao kipindi chote cha kampeni kitu ambacho ni kigeni kukiona katika mikutano ya upinzani na kinastahili pongezi za dhati kwa kuwa ni uzalendo.
Anasema kutokana na hilo, wanasiasa hao wa upinzani wamesaidia kushusha hatari ya kutokea kwa machafuko. Anawapongeza pia akisema kitendo chao cha kuridhika na matokeo ya uchaguzi kimeonesha ukomavu katika siasa safi na uzalendo kwa taifa kwani siasa ni kwa ajili ya watu na si watu kwa ajili ya siasa.
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) 2025/2026, Shahidu Iddy anawataka vijana kuachana na siasa za mihemko na hisia za mitandaoni badala yake, waungane na serikali kujenga taifa moja la watu wenye amani na utulivu.
“Vijana wenzangu wasitumike vibaya na makundi na watu wanaoishi nje ya nchi badala yake, watambue thamani yao katika kujenga na kuendeleza taifa lenye mustakabali bora wa vijana kwa maslahi ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” anasema Iddy.
Aidha, anawakumbusha vijana kutambua haki zao kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi. Kwamba, wanapaswa kutumia njia zilizoainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudai haki na kuwasilisha changamoto zao kwa njia zisizohatarisha amani na mshikamano wa taifa.
“Vijana lazima wajue kuwa taifa linatumia gharama kubwa kuwajenga ili wawe viongozi bora wa baadaye wa familia, jamii na nchi kwa ujumla, hivyo wasiendekeze kuhongwa fedha ili watumike katika siasa kutokana na umaarufu wao katika jamii,” anasema.
Anawahimiza jukumu lao katika ujenzi wa taifa linalozingatia utawala wa sheria lisilozingatia ubaguzi wa rangi, dini, ukabila wala ukanda na lenye watu wasio na mihemko.




Nowadays earning money online is very easy . Eanrs every month online more than $17k by doing very easy home based job in part time u can also do this simple online Job by visiting websiteMore Details For Us→→ http://www.job40.media