Zaidi ya Bil 33/-zatekeleza miradi ya jamii Mara

MKOA wa Mara umeendelea kunufaika na uwekezaji wa Sekta ya Madini baada ya kutekeleza zaidi ya miradi 398 ya maendeleo yenye thamani ya Sh Bilioni 33.81 katika wilaya zote ndani ya kipindi cha miaka minne, hatua inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi.
Akizungumza hivi karibuni kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Afisa Mazingira, Byalugaba Chakupewa alisema utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka migodi ya kati na midogo umeendelea kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali.

Amesema michango ya kampuni za uchimbaji madini imeendelea kusaidia miradi ya kijamii, ikiwemo Shilingi milioni 40 zinazotolewa na ZEM (T) Co Ltd katika Wilaya ya Butiama, Sh milioni 40 za Polygold kwa Halmashauri ya Musoma, na Sh milioni 125 zinazotolewa na MMG Gold Mine kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Seka, madarasa Kalusenyi, ofisi ya kijiji cha Kaboni pamoja na jiko la gesi katika Shule ya Sekondari Kasoma.
SOMA: Mara yachimba dhahabu ya Trilioni 8.8
Aidha, amesema kupitia mpango wa vijana wa Mining for the Brighter Tomorrow (MBT), vikundi 53 vyenye jumla ya vijana 1,998 vimepatiwa leseni za uchimbaji mdogo, hatua inayoongeza ajira na ushiriki wa vijana katika uchumi wa madini.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, amesema mgodi huo umetumia Sh bilioni 26 kutekeleza miradi ya jamii kuanzia mwaka 2019 hadi 2025.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imetenga Dola milioni 1.8 kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wanaoishi jirani na mgodi, sambamba na kulipa zaidi ya Sh bilioni 2 za mrabaha kila robo mwaka.

Amesema zaidi ya watoto 500 tayari wamenufaika na mfuko wa elimu wa mgodi huo, ingawa bado kuna changamoto ya baadhi ya jamii kushindwa kutambua vipaumbele vya maendeleo, hali iliyosababisha Barrick kuanzisha mpango mkakati wa miaka mitano unaolenga kushughulikia mahitaji ya msingi kama upatikanaji wa maji na barabara.
Uhadi amebainisha kuwa mgodi umejenga tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita 300,000 linalohudumia vijiji vikiwemo vya Matongo, Mjini Kati na Nyabichune.



