DC Mwaipaya awahamasisha wananchi kushiriki michezo

MTWARA: MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amewataka wananchi wilayani humo kuendelea kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu ili kuimarisha afya na kuleta mshikamano.
Hayo yamejiri wakati wa bonanza la michezo lililoambatana na zoezi la kucheki afya kwa jamii hiyo lililokutanisha timu nane za Kata ya Nanguruwe iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara lililoanza Novemba 12, 2025 na kutamatika Novemba 15 mwaka huu lililoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Baadhi ya timu hizo nane ikiwemo Tandika FC, bodaboda FC, Mtemba City, Mafundi FC, Ajax Ngorongoro FC, Ngome FC ambayo ilimenyana na Watumishi FC ya halmashauri hiyo kwenye fainali ya bonanza hilo huku Watumishi FC ikiibuka kidedea ya bao moja dhidi ya mpinzani wake Ngome FC aliyetoka kapa katika mchezo huo.

Zawadi mbalimbali zimetolewa kwa timu zote nane zilizoshiriki bonanza hilo ikiwemo mipira, majezi na zingine huku mshindi wa kwanza ambaye ni watumishi fc akijitwalia zawadi ya kombe, jezi, mbuzi na zingine.
‘’Kikubwa zaidi ndugu zangu muweze kufahamu dhana ya michezo, michezo ina imarisha afya lakini inaleta umoja, mshikamano na kufanya watu wawe wamoja na leo hii naamini watu wengi wameweza kufahamiana kupitia michezo hii hilo ni kubwa sana,’’amsema Mwaipaya.

Pia amelishukuru shirika hilo kwa kuamua kuandaa bonanza hilo ambapo lengo lao kubwa ni kuhakikisha kwamba wako pamoja na jamii hasa kufuatia uwekezaji mkubwa wa gesi asilia uliyofanywa na shirika hilo katika maeneo hayo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TPDC, Ally Mluge amesema lengo la bonanza hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha mahusiana baina na shirika na jamii na TPDC ni sehemu ya wanamtwara na kusini kwa ujumla.



