Tanzania kamili Manila Kombe la Dunia Futsal

TIMU ya Soka ya Taifa ya mpira wa Futsal imewasili salama mjini Manila, Ufilipino juzi, tayari kwa michuano ya fainali za kombe la dunia inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi leo.
Timu 16 zinatarajiwa kumenyana katika michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Tanzania iliyo kundi C pamoja na timu za Ureno, Japan na New Zealand, inatarajiwa kuanza kurusha kete yake keshokutwa dhidi ya Ureno kabla ya kucheza na Japan Novemba 26 na kumaliza na New Zealand Novemba 29.
Mratibu wa Maendeleo ya soka la wanawake wa FIFA, Latoya Dacosta alisema jana, maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo yapo tayari na wanatarajia kuwa na michuano mizuri kama inavyokuwa kwenye michuano mingine inayoandaliwa na shirikisho hilo.

“Ni michuano yetu ya kwanza, tunatarajia kuwa na tukio bora na huu hautakuwa mwisho, itaendelea kufanyika kama ilivyo kwenye michuano ya michezo mingine chini ya FIFA,” alisema.
Tanzania iliwasili mjini hapa ikitokea Jakarta, Indonesia ilipoweka kambi ya maandalizi ya wiki moja. Meneja wa timu hiyo, Mary Musiba alilieleza gazeti hili kuwa kikosi cha watu 25 kiliwasili salama mjini hapa na kwamba hakuna mchezaji mwenye majeraha ya kushindwa kucheza, atakapopewa nafasi na kocha.
“Mpaka sasa timu iko vizuri. Wachezaji wetu wana afya njema, hakuna mwenye majeraha, tunamshukuru Mungu. Kocha leo (jana) ameendelea na programu yake kama kawaida ya mazoezi, akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri,” alisema.

Kwa mujibu wa ratiba ya FIFA, leo ndio ufunguzi wa michuano hiyo ambapo timu nne zinatarajiwa kumenyana kwenye uwanja wa PhilSports Arena mjini Manila.
Mechi zitakazofungua dimba la michuano hiyo zitahusisha timu zilizo kundi A kwa Morocco kucheza na Argentina, kabla wenyeji Ufilipino hawajacheza na Poland.

Timu za kundi B zinatarajiwa kukutana kesho kwa Colombia kucheza na Canada na Hispania dhidi ya Thailand, huku kundi C na D zikitarajiwa kucheza mechi zake Jumapili kwa Japan dhidi ya New Zealand na Ureno dhidi ya Tanzania, huku Italia ikimenyana na Panama na Brazil na Iran.



