Serikali mguu sawa ujenzi Bandari ya Bagamoyo

SERIKALI imesema inajiandaa kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema serikali inaanza ujenzi huo na kwamba wawekezaji wakija watajumuika nao na wasipokuja serikali itasimama yenyewe. Msigwa alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema bandari hiyo itakuwa na gati lenye kina cha meta 20 na akabainisha kwamba mitambo kwa ajili ya ujenzi huo ipo njiani inaletwa. Msigwa alisema bandari hiyo itakuwa ya aina yake katika ukanda wa Mashariki na itakuwa na magati 28 na kwa kuanzia magati 14 yatajengwa katika awamu ya kwanza. “Hii ni bandari ambayo inaweza kupokea na kuhudumia meli kubwa inayoweza kubeba makontena elfu 25 niwambie watanzania mambo yetu si mabaya,” alisema.
Msigwa amesema serikali imejipanga kuboresha bandari zote nchini ili mizigo inapofika katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara iweze kufika kwa urahisi katika nchi jirani. “Tunataka Bandari ya Dar es Salaam ifikie Congo, Burundi, Rwanda, Uganda, Zambia na Malawi. Ufanisi wetu umeongezeka maradufu na sasa tumekuwa tishio kwa washindani baada ya kuingia ubia na kampuni ya DP World,” alisema.

Msigwa amesema maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia mizigo kutoka tani milioni 21 hadi milioni 32 ndani ya kipindi cha miaka mitatu na mapato ya bandari yameongezeka kutoka Sh bilioni 900 na kufikia zaidi ya Sh trilioni moja.
Amesema muda wa meli kusubiri kushusha mizigo katika bandari hiyo umepungua kutoka siku 46 hadi siku saba kwa meli zenye mzigo mchanganyiko, na zile zenye kontena zinashusha na kuondoka mara moja. Msigwa alisema hatua hiyo imechochewa na ubia na DP World ambao umeokoa zaidi ya Sh bilioni 400 zilizokuwa zikitumika kuendesha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), fedha ambazo sasa zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo afya.
Aidha, amesema serikali inalenga hadi kufikia 2029 kuhudumia tani milioni 50 kupitia bandari nchini, ikilinganishwa na tani milioni 32 zinazohudumiwa sasa. Kuhusu Bandari ya Tanga, Msigwa amesema serikali imejenga bandari ya Kisiwa Mgao ambayo itahudumia mizigo michafu kama makaa ya mawe, chuma na saruji.

Amesema pia gati mbili zimeongezwa na kuifanya bandari hiyo sasa kuhudumia hadi tani milioni moja na nusu, na kufikia mwishoni mwa mwaka huu inatarajiwa kufikia tani milioni mbili, huku lengo ikiwa kuhudumia tani milioni tatu kwa mwaka.
Katika hatua nyingine, Msigwa amesema bandari za Bukoba na Kemondo zimekamilika, wakati Mwanza Kaskazini ipo mbioni kukamilika ili kuhudumia mzigo wa Uganda kupitia Tanzania kwa asilimia 38 kutoka asilimia tatu za awali. SOMA: Serikali: Ni vita ya uchumi



