Serikali: Ni vita ya uchumi

SERIKALI imesema taarifa za kupotosha kuhusu matukio ya vurugu wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu na siku zilizofuatia zina lengo la kuharibu uchumi wa Tanzania. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema si haki na si sawa kwa chombo cha habari kuchapisha taarifa za upande mmoja na kisha kutoa sababu kuwa maofisa wa serikali walipotatufwa hawakupatikana. Msigwa amesema taarifa za kwenye vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ni njia ya kupita tu ili lengo lao ni kuharibu uchumi wa Tanzania. “Wanataka kuharibu biashara zetu, wanataka kupunguza watalii ili tukose fedha na kibaya zaidi ni kutaka Tanzania iadhirike ili washindani wetu wa kibishara wanufaike,” alisema Msigwa.
Amesema serikali inaendelea kuhakiki maudhui ya makala ya CNN na kwamba chombo hicho kimefanya makosa ya kiuadilifu na kiweledi katika uandishi wa habari kwa kuchapisha na kutangaza maudhui yanayoegemea upande mmoja. “Si kweli kwamba CNN ilishindwa kupata maudhui kutoka upande wa serikali kwa ripoti zao zote wanazozitoa za upande mmoja.
Inashangaza kuona chombo cha habari za kimataifa kama CNN kufanya makosa makubwa ya kimaadili kama haya ambayo yamefanywa,” alisema Msigwa. Ameongeza: “Natoa wito kwa CNN waje upande wa serikali wasikilize na wakachapishe maudhui yenye usawa, ukweli na yasiyokuwa na mgongano wa maslahi. Waache kuchagua kuripoti upande mmoja wakati upande mwingine wameunyima nafasi, si sawa”.
Msigwa amesema anafahamu mwandishi wa habari wa CNN aliyeandika makala hiyo hakuwa Tanzania na aliandaa makala kwa kutumia picha zilizopigwa kwa simu wakati wa vurugu bila kuwasiliana na mamlaka zinazohusika Tanzania.
“Amekwenda kuandaa makala ya upande mmoja… serikali inatoa wito kwa CNN kuzingatia maadili na weledi katika uandishi wa habari na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa zisizokuwa na vyanzo halali na rasmi na kupotosha kuzua taharuki,” alisema Msigwa.
Ameongeza: “Sishabikii vifo vilivyotokea, wote sisi ni Watanzania, wote tumesikitishwa sana na matukio hayo, hakuna anayeyashabikia, lakini kwa nini chombo cha habari kifanye kazi ya kutengeneza maudhui ya uchochezi yanayoongeza machungu kwa wananchi, yanayoongeza hasira kwa wananchi”.
Msigwa amesema baada ya matukio ya siku chache na katika miji michache Tanzania ipo shwari na Watanzania wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. “Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kuhakikisha watu na mali zao wanabakia kuwa salama na matisho yote ya kiusalama yanakabiliwa ipasavyo,” alisema.
Katika maelezo yake, Msigwa amesema shughuli za kiuchumi zinaendelea vizuri na Tanzania ni moja ya nchi chache ambazo zinakwenda kupiga hatua kubwa za kiuchumi kupitia miradi mikubwa na ya kimkakati. “Miradi hii ya kimkakati ndio inalaza watu na viatu. Na wale vijana wetu ambao wameingia kwenye kampeni ya kufanya ushabiki wa kuichafua Tanzania wanacheza ngoma ya watu wengine.
Mengine wakiendelea kusema tutasema kinachoendelea si kwamba hatujui tunajua,” alisema. Ametoa mwito kwa vyombo vya habari viache kuingilia uchunguzi wa tume iliyoundwa kuchunguza matukio ya Oktoba 29, na Watanzania waendelee kuilinda nchi yao kwa wivu mkubwa. SOMA: BoT yatoa hakikisho usalama mifumo ya malipo



