Siku 7 Kukamilisha Barabara ya Gairo–Kintinku

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa siku saba kwa wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi ya dharura katika barabara ya Gairo – Dodoma – Kintinku wakamilishe kuweka tabaka la juu la lami.

Ulega ametoa maelekezo hayo mkoani Dodoma juzi wakati akikagua utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea na ile iliyokamilika katika maeneo ya Mbande, Mtanana, Pandambili na Silwa Mkoani humo na kuridhishwa kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maeneo yote. Ulega amewataka wakandarasi hao wafanye kazi usiku na mchana na kukamilisha kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Ameuelekeza uongozi wa Wilaya ya Kongwa uendelee kuimarisha ulinzi wakati wote wa utekelezaji wa mradi. “Nimekagua na nimeona athari za mvua zinazonyesha kutoka mikoa jirani ya Manyara, ninatoa wiki moja kwa wakandarasi kukamilisha kazi hiyo ili mvua hizi zinapoanza kunyesha mkoani Dodoma isikute wananchi bado wapo kwenye barabara ya mchepuo,” alisema Ulega.

Aidha, ameelekeza wakandarasi hao wakamilishe kazi zingine zilizobaki zikiwemo za ufungaji wa taa 300 za barabarani na kuweka alama za barabarani wakati magari yakiendelea kupita katika barabara hiyo.

Wakandarasi hao ni Kings Builder Company anayetekeleza ujenzi wa makalavati makubwa katika eneo la Mbande na Technics Construction Group anayetekeleza ujenzi wa makalavati maeneo ya Pandambili na Silwa katika barabara hiyo.

Ulega amewataka wakandarasi wazawa watekeleze kazi zao vizuri kwa kuwa ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wizara kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa wenye uwezo, utayari na ubora wa kazi zao.

“Tunayo maelekezo ya kuwapeni kazi nyingi za ujenzi lakini hatuwezi kuwapa tu kama hamfanyi kazi nzuri, jitahidini kufanya kazi nzuri kwa wakati na ubora,” alisema. Ulega amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa makalavati makubwa na unyanyuaji wa tuta la barabara eneo la Mtanana kazi inayofanywa na mkandarasi Estim Construction kwa gharama ya Sh bilioni 26.

Ameahidi kulifanyia kazi suala la kuongezewa upana wa barabara kwa ajili ya wananchi kufanya biashara. Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dodoma, Zuhura Amani ameeleza utekelezaji wa ujenzi wa makalavati na unyanyuaji wa tuta la barabara katika eneo la Mbande umefikia asilimia 88 na unagharimu Sh bilioni 7.9.

Zuhura ameeleza asilimia 95.4 zimefikiwa katika utekelezaji wa mradi wa makalavati makubwa na unyanyuaji wa tuta la barabara eneo la Pandambili na Silwa na mradi ni wa Sh bilioni 2.8. SOMA: Serikali kuongeza bajeti ya TARURA

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button