Vita ya Pacome, Feisal, Ahoua yaahirishwa

DAR ES SALAAM; TUZO za TFF msimu wa mwaka 2024/25 zilizokuwa zifanyike Desemba 5, mwaka huu zimeahirishwa.
Taarifa iliyosainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo imeeleza kuwa uamuzi huo unatokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Ijumaa iliyopita TFF ilitoa orodha ya wanamichezo wa makundi mbalimbali watakaowania tuzo hizo. Makundi hayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho, Ligi Kuu ya Wanawake, Tuzo za Utawala na Tuzo za Ligi nyingine.

Kwa upande wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora ni Dickson Job, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wote kutoka Yanga, Jean Ahoua (Simba) na Feisal Salum (Azam).



