DStv kunogesha AFCON kwa Kiswahili

DAR ES SALAAM; MICHEZO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) itatangazwa kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili.

Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo na Mkuu wa Masoko wa DStv Tanzania, Ronald Shelukindo, wakati wa uzinduzi wa kampeni iitwayo ‘Wanafamilia Tuna Kikao, Chimbo ni SuperSport’.

Amesema DStv itaonesha mechi zote 52 za michuano hiyo kupitia chaneli ya Supersport, ambapo Tanzania ‘Taifa Stars’ ni miongoni wa timu zitakazoshiriki katika michuano hiyo itakayofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.

Amesema matumizi ya Kiswahili katika matangazo yatasaidia mashabiki wa Afrika Mashariki kupata ufahamu mpana zaidi wa michezo na kuwafanya wahusike moja kwa moja na matukio yanayoendelea uwanjani.

Katika kuongeza wigo wa utazamaji, kampuni za Canal+ na SuperSport zimethibitisha kuonesha mbashara michuano yote ya CAF TotalEnergies Morocco 2025, ambayo inatajwa kuwa miongoni mwa michuano mikubwa na yenye ushindani zaidi katika historia ya Afrika.

Taarifa ya pamoja ya CAF, Canal+ na SuperSport imeeleza kuwa Canal imepata haki za urushaji katika nchi zinazotumia lugha za Kifaransa, Kiingereza, Kireno na lugha mbalimbali za Kiafrika, huku SuperSport ikihudumia zaidi mashabiki wa Afrika Mashariki, Kusini na maeneo mengine ya bara hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button