Meya mpya Ilemela aahidi amani, umoja

MWANZA; MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamemchagua Sarah Ngw’hani, ambaye Diwani wa Kata ya Buswelu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa meya mpya wa manispaa hiyo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Desemba 2, 2025 viwanja vya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela., Ngw’hani alipata kura 27 za ndiyo kati ya kura 27 zilizopigwa.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, meya huyo aliwashukuru madiwani wote kwa kumuamini na kumuunga mkono na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika nafasi ya Naibu Meya, Kuluthum Abdallah(CCM) alishinda uchaguzi huo baada ya kupata kura 23 na kumuangusha mpinzani wake Donald Ndaro wa ACT Wazalendo. Jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 27.
Kwa upande wake Kuluthum Abdallah ambaye ni Diwani wa Viti Maalum (CCM), alisema baraza la madiwani litafanya kazi kwa karibu na Mkurugenzi wa Manispaa Ummy Wayayu, ili kushauri Manispaa hiyo na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali.



