Watanzania wasilisheni taarifa za vurugu

TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeanza rasmi kazi zake. Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Novemba 19, mwaka huu ikiwa na wajumbe wengine saba ambao ni Watanzania wabobezi katika masuala mbalimbali.
Majukumu ya tume hiyo ni pamoja na kuchunguza chanzo cha machafuko ya Oktoba 29, mwaka huu, kuwabaini waliohusika, kutathmini madhara yaliyojitokeza na kupendekeza hatua za kuimarisha amani, usalama na umoja wa kitaifa.Katika taarifa yake kwa umma, tume imewaita wananchi watoe taarifa, ushahidi, maoni na mapendekezo yatakayosaidia katika uchunguzi wake.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu mstaafu Chande, mafanikio ya kazi hiyo yatategemea ushirikiano wa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kubainisha ukweli.Tungependa kusisitiza umuhimu wa Watanzania wenye taarifa kama ambavyo tume imeeleza, kujitokeza na kuziwasilisha kwao ili kusaidia katika kuhakikisha tume inakuja na majawabu ya nini hasa kilichotokea Oktoba 29, mwaka huu.
Watanzania wote wanafahamu kilichotokea siku hiyo lakini hawana majawabu ya yale ambayo tume imepewa kama hadidu za rejea kuja na majawabu yake; chanzo cha machafuko, wahusika, madhara na kuja na mapendekezo ya nini kifanyike ili hali kama hiyo isirudie tena na hatua za kuchukua.
Kwa msingi huo, sisi tunaamini taarifa hizo kutoka kwa Watanzania, zitasaidia katika kuliponya na kuliepusha taifa kuingia katika machafuko kama ya Oktoba 29, hivyo wajitokeze bila kusita kwenye tume kutoa ushirikiano unaohitajika. SOMA: Tuipe ushirikiano Tume ya Uchunguzi
Tuna imani kubwa na tume kutokana na ukweli kuwa imeundwa na watu wanaoheshimika na wenye rekodi zilizowapa heshima ndani na nje ya nchi, hivyo suala la kufanya kazi kwa weledi kwao halina mjadala na pia tayari wamesema taarifa za watakaojitokeza zitakuwa siri na wasiotaka kutambuliwa watalindwa.
Tume imepewa siku 90, hivyo wote wanaotaka kutoa taarifa kwa tume hiyo ni lazima wazingatie muda huo ili kurahisisha kazi ya tume kufanyika ndani ya muda husika hasa ikizingatiwa Watanzania wanasubiri majawabu yake kwa mustakabali wa nchi.Tumefurahishwa pia na ukweli kuwa tume imeweka njia mbalimbali za kupokea taarifa au ushahidi kwa wale walionao, hivyo si wote ambao watalazimika kwenda kutoa taarifa zao ana kwa ana.
Tutumie njia hizo kupeleka taarifa na ushahidi kwa nia ileile ya kuijenga Tanzania yetu, na kuliponya taifa dhidi ya madhila ya Oktoba 29. Kama alivyoeleza Rais Samia hivi karibuni alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam, Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe, hivyo tutumie tume hii kulijenga taifa na kulisaidia kusonga mbele kama taifa la amani, umoja na mshikamano.



