Rais Mwinyi apokea Tuzo ‘Africa’s Best Corporate Retreat 2025’

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya utalii kuongeza ushirikiano ili Zanzibar na Tanzania kunufaika zaidi na tuzo na fursa za kimataifa.
Tuzo ya Africa’s Best Corporate Retreat Destination 2025 ilikabidhiwa kwa Rais Mwinyi tarehe 12 Desemba 2025 Ikulu Zanzibar, baada ya Zanzibar kushinda kwenye World Travel Awards 2025 yaliyofanyika Bahrain, ikishindana na Kenya, Afrika Kusini, Morocco na Botswana.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Mwinyi amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwa Zanzibar na Tanzania, ukionyesha maendeleo makubwa ya sekta ya utalii. Hatahivyo amesisitiza kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha vivutio, na kutumia tuzo kama chachu ya ushindani wa kimataifa, hasa katika utalii wa mikutano na matukio.
Rais Mwinyi pia amebainisha kuwa utalii ni “sekta mama” ya uchumi wa Zanzibar, na kuhimiza mipango thabiti na ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau kuongeza thamani na mapato. Ameongeza kuwa maandalizi ya pamoja yanahitajika kuelekea Tanzania kuwa mwenyeji wa World Travel Awards Grand Final 2026, huku akihimiza ubunifu na kuboresha bidhaa na huduma za utalii.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, amesema ushindi huu unaweka Zanzibar kwenye ramani ya dunia kama kitovu kipya cha utalii wa safari barani Afrika. Ameongeza kuwa Tanzania imeibuka na tuzo tano kwenye mashindano hayo, ikiwemo Tanzania World’s Leading Safari Destination. SOMA: Tanzania yang’ara tuzo za utalii Afrika



