Serikali yajizatiti kukabili upungufu wa maji Dar, Pwani

DAR ES SALAAM: Serikali itaendelea kuchukua hatua zote za dharura kuhakikisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani inaendelea kupata huduma ya maji kwa kadri inavyowezekana, ikiwa ni pamoja na kutumia kikamilifu visima vyote vya maji vilivyopo katika eneo la Kigamboni.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, mara baada ya kutembelea na kukagua hali ya ufanyaji kazi wa visima vya maji vya Kigamboni jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji inayojitokeza hususan katika kipindi cha kiangazi.

Waziri Aweso amesema serikali imejipanga kuhakikisha wananchi hawaathiriki zaidi na upungufu wa maji kwa kuchukua hatua za haraka, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa maji kupitia vyanzo vilivyopo na kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya maji ili huduma iendelee kupatikana kwa ufanisi.
Akizungumzia mipango ya muda mrefu ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Waziri Aweso amesema serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu iliyopo na utafutaji wa vyanzo vipya vya maji, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa uhakika na endelevu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Dalmia Mikaya, ameelezea hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo, akibainisha kuwa serikali kwa kushirikiana na mamlaka husika inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na za kati ili kupunguza adha inayowakabili wakazi wa Kigamboni.

Naye Mbunge wa Kigamboni, Halan Sanga, akizungumza kwa niaba ya wananchi, ameishukuru serikali kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na tatizo la maji, huku akiomba hatua za haraka na za kudumu kuendelea kuchukuliwa ili kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa maji katika eneo hilo.



