TANZANIA imepiga hatua kubwa katika sekta ya anga, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya abiria waliotumia viwanja vyake vya ndege hadi milioni 6.8 mwaka 2023 kutoka milioni 2.8 mwaka 2020.
Kabla ya janga la Covid-19, idadi ya abiria waliokuwa wanatumia viwanja vya ndege vya nchi ilikuwa milioni 5.6 lakini ilishuka kwa asilimia 50 kutokana na vizuizi vilivyoyakumba mataifa mengi.
Hata hivyo, hali imeimarika na kufikia mwaka 2024 idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 7.8.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi kama sehemu ya kusherehekea miaka 80 ya Mkataba wa Chicago mkoani Dar es Salaam.
Siku hiyo ambayo inasherehekewa kila Desemba 7, ilihusisha utoaji wa vyeti kwa wahitimu wanane wa Tanzania, wakiwemo marubani na wahandisi wa ndege waliokamilisha masomo yao wakiwa wamesomeshwa kupitia Mfuko wa Mafunzo wa TCAA ambao miongoni mwao watatu ni wanawake.
Msangi alisema hatua hiyo katika sekta ya anga imefikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika nchini, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa usalama wa anga na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya nne Afrika kwa kupata asilimia 88 mwaka jana katika programu ya kimataifa ya kupima usalama ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
“Hii inaonesha sekta ya anga nchini inakua kwa kasi kwa sababu inasimamiwa vyema. Serikali imefanikiwa kununua na kufunga mifumo minne ya rada kote nchini, ambayo inatufanya tuweze kufanya uangalizi wa kitaifa na kufuatilia anga yetu yote,” alisema.
Alisema kabla ya kuwa na mifumo ya rada, asilimia 25 ya anga zilikuwa zinatufuatilia lakini sasa kwa vifaa bora, nchi ina uwezo wa kuhudumia nchi nyingine kama anga ya Burundi ambayo inafuatiliwa kutoka urefu wa futi 24,500.
Msangi alisema kupitia kamati ya kitaifa na Mpango wa Kuzuia na Kudhibiti Matukio ya Afya ya Umma katika Usafiri wa Anga (CAPSCA), Tanzania imefanikiwa kudhibiti kuenea kwa haraka kwa magonjwa yanayoambukiza, kama vile M-Pox katika viwanja vyake vya ndege na ndiyo sababu kumekuwepo na maendeleo makubwa katika ongezeko la idadi ya abiria.
Hadi sasa kuna mashirika 46 ya ndege ya Kitanzania yaliyosajiliwa na mengine 23 ya kimataifa yanatoa huduma katika viwanja vikuu vitatu vya ndege nchini vilivyopo Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar na viwanja vingine vinne vinatarajiwa kuongezwa hivi karibuni.
Alisema serikali imeingia mikataba ya huduma za ndege na zaidi ya nchi 88 ambazo zinawezesha pande zote mbili kufanya kazi katika mataifa washirika katika sekta ya anga.
“Tunatambua juhudi ambazo serikali inafanya kupanua ndege zetu. Kufikia mwaka 2016, tulikuwa na ndege moja tu inayoweza kubeba abiria 50, serikali imenunua ndege nyingine na sasa tunazo ndege 16, ikiwemo ndege moja ya mizigo,” alisema.
Msangi alielezea changamoto ambazo bado zinaikumba sekta hiyo zikiwa ni pamoja na ukosefu wa utaalamu wa ndani kwa marubani na wahandisi wa ndege, akisema kuwa kati ya marubani 700, takribani 350 ndiyo wazawa na kwamba kuna upungufu wa marubani wapatao 150 katika sekta hiyo.