LUANDA, Angola: Serikali ya Afrika Kusini imeendelea kutambua na kuuenzi mchango wa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo na bara la Afrika kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Candith Mashego-Dlamini wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC uliomalizika Machi 11, 2024 jijini Luanda, Angola.
Akizungumza kwenye agenda ya Sanamu ya Hayati Mwl Nyerere iliyozinduliwa rasmi Februari 18, 2024 jijini Addis Ababa, Ethiopia, Dlamini alieleza kuwa uzinduzi wa sanamu hiyo ni ishara muhimu ya kuenzi jitihada na mawazo yake ambayo yataendelea kukumbukwa daima.
Aidha, alieleza kuwa Tanzania kupitia Mwl. Nyerere iliweka bayana nia ya dhati na ya wazi ya kuzikomboa Nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika Kusini.
Tanzania ndio ilikuwa kimbilio la kwanza kwa Afrika Kusini baada ya kutokea kwa mauaji maarufu ya “Sharpeville massacre” yaliyotokea Machi 21, 1960
Kwa upande wa SADC, Dlamini amemwelezea Mwl. Nyerere kuwa ni miongoni mwa viongozi waanzilishi wa SADCC mnamo mwaka 1980 na baadae SADC.