Aga Khan, Tapo kuzindua kampeni ya kitabibu

HOSPITALI ya Aga Khan Tanzania kwa kushirikiana na Tanzania Women Tapo (TWT) wanatarajia kuzindua kampeni ya Taifa ya Samia afya kwa wanawake wa masokoni na wachuuzi kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa afya bure kwa wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mkuu wa wa Aga Khan Tanzania Sisawo Konteh amesema kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Jumanne Desemba 10, 2024 kwenye Viwanja vya Mnazimmoja.

Amesema wanatarajia kufanya uchunguzi wa magonjwa ya saratani, shinikizo la damu na sukari na kwamba wamejitoa kama taasisi ili kuwafikia wanawake wengi walioko mitaani na kuwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi siku hiyo.

Advertisement

“Huu ni mmoja ya ushirikiano tulioutafuta kwa muda mrefu kuhakikisha tunawafikia wanawake wengi. Sio mara ya kwanza kufanya shughuli hizi, tuna vituo katika mikoa mbalimbali vinavyotoa huduma, na tutaendelea”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Women Tapo Lulu Yassin amesema wanataka kuwagusa wanawake ambao sio wauzaji tu ni wajasiriamali, mama, viongozi wa jamii, na wanamapinduzi wa kimya wa nguvu ya kiuchumi wa taifa.

“Kazi yetu haijawa ya kutoa misaada tu. Imekuwa kuhusu heshima. Kuutambua uwezo wa kushangaza uliomo ndani ya kila mwanamke anayeamka kabla ya machweo kufungua biashara yake, anayepambana na changamoto za kiuchumi, na anayeendelea kusaidia familia yake kwa uadilifu usio na kipimo. Kampeni ya Afya kwa Wanawake wa Masokoni na Wachuuzi ni ushuhuda wa kujitolea.


kwetu,

“Hii si mpango wa afya tu. Ni mpango wa kina wa matumaini na mabadiliko. Tunalenga kuwafikia wanawake 1,000 katika kila mikoa yote 31 ya Tanzania – yaani kugusa maisha ya takriban wanawake 31,000 wa masokoni na wachuuzi,”amesema.

Amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kujumuika nao , kuangalia macho yao na kusikiliza hadithi zao za ustahimilivu, kufahamu changamoto zao na ndoto zao.

Amesema kampeni hiyo ya kitabibu si mpango wa afya tu – ni jukwaa la hawa wanawake kutambuliwa kama wachangiaji muhimu wa kiuchumi.

Mkurugenzi wa Marcus Mwemezi Foundation (MMF) Belinda Nendiwe amesema anashukuru kuwa sehemu ya kampeni hiyo kwani wamepanga kutoa elimu ya Afya ya akili kwa wanawake hao.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu mkoa Dk Ayoub Kibao amesema serikali inaunga mkono mradi huo na itaendelea kuja na miradi mingine itakayowanufaisha wanawake.

Mwisho