Kampeni yazinduliwa kuokoa watoto wenye matatizo ya moyo

DAR ES SALAAM: HEART Team Africa Foundation (HTAF), kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imezindua rasmi kampeni ya “Kutoa Ni Moyo”, kampeni ya kitaifa inayolenga kuchangisha fedha na kuongeza uelewa kuhusu watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo nchini Tanzania.
Kampeni hiyo inalenga kuwaunganisha Watanzania kutoka makundi mbalimbali ya jamii ili kusaidia watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo kupata matibabu na huduma muhimu za afya ya moyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema tatizo la magonjwa ya moyo kwa watoto linaendelea kuwa changamoto kubwa nchini na linahitaji mshikamano wa kitaifa.

“Nchini Tanzania, zaidi ya watoto 16,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na matatizo ya moyo. Hii ina maana kuwa kila siku kuna familia zinazopokea taarifa zinazoweza kubadilisha kabisa maisha ya watoto wao,” amesema Dk Kisenge.
Amesema takribani watoto 4,000 wanahitaji upasuaji wa moyo kwa haraka, huku akibainisha kuwa kwa familia nyingi muda ni sawa na maisha.
“Kupitia kampeni ya Kutoa Ni Moyo, tunatoa wito kwa Watanzania wote, taasisi binafsi, mashirika na taasisi za serikali kushiriki katika harakati hizi za kuokoa maisha ya watoto kwa kuingia kwenye tovuti ya kutoanimoyo.chapaa.co.tz,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HTAF, Dk Naizihijwa Majani, amesema kampeni hiyo imelenga si tu kuchangisha fedha bali pia kujenga uelewa wa muda mrefu kuhusu afya ya moyo na umuhimu wa jamii kushiriki kusaidia watoto wenye changamoto hiyo.

“Tanzania ina utamaduni mkubwa wa mshikamano na kusaidiana. Kutoa Ni Moyo inabadilisha michango midogo ya mtu mmoja mmoja kuwa nguvu kubwa ya kitaifa yenye matokeo makubwa. Hii si kampeni ya kuchangisha fedha pekee, bali ni harakati inayojengwa juu ya huruma, umoja na imani kuwa kuokoa maisha ya mtoto ni jukumu letu sote,” amesema Dk Majani.
Kwa mujibu wa takwimu za afya duniani, magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.9 kila mwaka na kuwa chanzo kikubwa zaidi cha vifo duniani.
Aidha, takwimu zinaonesha kuwa mtoto mmoja kati ya watoto 100 huzaliwa akiwa na tatizo la moyo.
“Hakuna mzazi anayepaswa kuona mtoto wake akiteseka kwa sababu tu hana uwezo wa kugharamia matibabu, ” amesisitiza Dk Majani.
Kampeni hiyo inalenga kukusanya shilingi bilioni 25 kupitia ushiriki wa wananchi, makampuni, wadau wa maendeleo, taasisi mbalimbali, diaspora, watu maarufu, jumuiya za michezo pamoja na jamii kwa ujumla.
Fedha zitakazopatikana zitatumika kugharamia upasuaji na matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, uchunguzi wa mapema, programu za elimu ya afya ya moyo pamoja na kusaidia familia zinazokabiliwa na changamoto hiyo.
Aidha, kampeni hiyo itatumia teknolojia ya kidijitali na mifumo ya kuchangisha fedha mtandaoni ili kurahisisha Watanzania kuchangia kwa uwazi na urahisi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Juhudi za awali za uchangishaji zilizofanywa na wadau na washirika tayari zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.08 kupitia fedha taslimu na misaada ya vifaa, jambo linaloonyesha moyo wa Watanzania kusaidiana katika kuokoa maisha.



