Agizo kutengeneza kumbi za wabunifu chipukizi lina tija

HIVI karibuni serikali iliiagiza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) itengeneze na kuboresha kumbi kwa ajili ya wabunifu chipukizi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo ndiye aliyetoa maagizo hayo kwa niaba ya serikali wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za Costech zinazojengwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) jijini Dodoma.
Tunaunga mkono utekelezaji, tena wa mapema wa agizo hilo kwa kuwa tunaamini kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani, hitaji la utafiti na ubunifu ni la lazima kwa maendeleo ya taifa.
Tunaamini kama alivyoeleza Profesa Nombo, kuwepo kwa kumbi hizo kwa wabunifu kutasaidia kuwaendeleza vijana kwenye bunifu walizobuni ili waweze kuzitangaza na kuingia katika soko la biashara la kitaifa na kimataifa.
SOMA: Kazi za ubunifu, uvumbuzi zisiishie kwenye maonesho
Kwa mfano, sasa hivi Serikali ya Awamu ya Sita imeweka nguvu kubwa katika kuimarisha ujuzi, hasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu na vya kati na kupitia ujenzi wa vyuo vya ufundi katika wilaya nchini, hatua kubwa imefanyika.
Hivyo, tunakazia hili agizo la Profesa Nombo kwa Costech kwa kuwa limekuja kwa wakati muafaka ambapo nchi inapambana kupunguza tatizo la ajira kwa kuhakikisha Watanzania walio katika soko la ajira, hasa vijana wanajiajiri na kuajiriwa.
Tunaamini wahitimu wa vyuo vya ufundi nchini kama Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na vinginevyo watapata mahali sahihi pa kuongeza ubunifu na ujuzi wao kwa vitendo na hivyo kusukuma mbele maendeleo yao na ya nchi.
Yapo mataifa kama China na India yaliopiga hatua kubwa kama hii inayofanywa na Serikali ya Tanzania sasa kwa kuwekeza kwenye ubunifu na ujuzi, hasa wa elimu za ufundi na wamepiga hatua kubwa kiuchumi.
Tunaamini kumbi hizi za ubunifu zikikamilika zitawawezesha vijana kufanya mazoezi ya vitendo katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanakuwa bora darasani na nje kwenye mazoezi ya vitendo.
Tayari Costech wameeleza bayana kupitia Mkurugenzi wake, Dk Amos Nungu kwamba kumbi zitakazojengwa zitatumika kuendeleza bunifu.
Kwa mujibu wa Costech, wabunifu hao watalelewa kwa miaka miwili na tume hiyo na baadaye watahitimu kwa ajili ya kwenda kuanzisha kampuni zao ikiwemo kujiajiri na kuajiri wengine.
Tunaiona Tanzania mpya kisayansi na teknolojia katika miaka michache ijayo, hasa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kwenye sekta ya sayansi nchini.
Ujio wa kumbi za kuendeleza wabunifu ni fursa inayopaswa kuchangamkiwa na Watanzania wote, hasa vijana kwa sababu ni njia sahihi na yenye tija ya kupambana na umaskini.



