Agizo la udhibiti bidhaa viwandani lizingatiwe

KATIKA moja ya eneo ambalo Watanzania wamekuwa wakilalamikia ni ubora wa bidhaa zinazozalishwa iwe ndani au nje ya nchi.
Kwa muda sasa, kumekuwapo na malalamiko kwamba baadhi ya bidhaa zinazoingizwa sokoni zimekuwa na ubora usiokidhi viwango na hivyo kuhatarisha sio tu watumiaji wa bidhaa hizo, bali pia kuchafua jina la nchi na kampuni husika.
Kumekuwapo na kutupiana lawama kati ya taasisi ambazo zinahusika na kuangalia ubora wa bidhaa mbalimbali, linapokuja suala la ubora wa bidhaa hizo hasa pale zinapogundulika kuwa zilizopo sokoni hazikidhi viwango.
Tumefurahishwa na agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) akilitaka liende viwandani kukagua na kudhibiti ubora wa bidhaa.
Majaliwa alisema hayo Dodoma wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Viwango ambalo litakuwa makao makuu ya TBS. Jengo hilo lenye thamani ya Sh bilioni 25.3 linajengwa eneo la Njedengwa.
Kwa mujibu wa Majaliwa, ni muhimu TBS waanze kwenda viwandani kwa wazalishaji ili kudhibiti ubora wa bidhaa kumsaidia mzalishaji kufahamu anachozalisha ni bora au la, kisha asaidiwe kuboresha au kuacha uzalishaji mapema badala ya kuingia hasara ya uwekezaji wake.
Pia, alisema pia kufanya hivyo si tu kutamsaidia mzalishaji bali pia kutaokoa afya za Watanzania na walaji na kuwa serikali inataka kuona bidhaa zinazozalishwa zinakidhi ubora na kuwa na nembo ya ubora zipate soko la ndani na nje.
Tunaungana na Waziri Mkuu kulikaribisha agizo hili tukiamini kwamba kama litatekelezwa kikamilifu, basi litaondoka kabisa kama sio kupunguza bidhaa zisizo na ubora zinazoingia sokoni.
Tunasema hivyo kwa sababu kama ukaguzi utafanyika mapema na kwa kuzingatia sheria na kusimamia viwango vya uzalishaji, basi hakutakuwa na mzalishaji anayepata hasara au mwananchi atakayeathiriwa na kupata bidhaa isiyokidhi viwango.
Tunaamini TBS wana uwezo wa kufanya kazi hii, na kama uwezo huo haupo, kwa majukumu yao na kwa sheria zao, wana uwezo wa kushauri mamlaka kuona jinsi gani kazi hii itatekelezwa ili bidhaa zinazozalishwa zikidhi viwango na viwe shindani kwa soko la ndani na nje ya nchi.
Na hili litasaidia sana katika kuimarisha ustawi wa wananchi kwani watapata bidhaa zenye ubora na hivyo kuimarisha afya zao, lakini pia kwa bidhaa nyingine tofauti na za vyakula, maana yake zitaenda kuleta matunda bora kwani zitakuwa zimezalishwa kwa viwango vinavyowekwa na hivyo kuwa salama kutumika nchini na nje ya nchi.
Kwa hiyo, ni vyema TBS kuanza mara moja utekelezaji wa agizo hilo kwani lina mchango mkubwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi kwani afya njema ni mtaji katika ufanyaji kazi, lakini pia bidhaa bora zinachangia katika kuongeza mapato ya nchi kwa kuingiza fedha za ndani na zile zinazopatikana kwa mauzo ya nje.