MAHAKAMA ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa Kijiji cha Inalo wilayani humo, Isacka Ngwesa (49) kwa kosa la kumnajisi mtoto wa miaka minane.
Shauri la kesi hiyo ya jinai namba 29213 la mwaka 2024, lilikuwa chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Lucas Gambago ambapo mbali na adhabu hiyo mshitakiwa alitakiwa kumlipa fidia ya Sh 500,000 muathirika.
Awali, akisoma maelezo ya kosa mbele ya mahakama, mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashitaka wilaya hiyo, Edwine Evarist alieleza Oktoba 3, 2024 katika Kijiji cha Inalo wilayani humo mshitakiwa alimnajisi mtoto huyo.
Evarist alisema mshitakiwa baada ya kutenda kosa hilo alikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Lagangabilili ambapo alihojiwa kisha kufikishwa mahakamani.
Mashahidi sita walitoa ushahidi huo katika kesi hiyo na vielelezo viwili vilitolewa na upande wa mashitaka kama ushahidi, ambapo mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza.
Baada ya kupewa nafasi ya kujitetea, Hakimu Gambago alisema mahakama imemkuta na hatia, hivyo atatumikia kifungo cha maisha jela na kumlipa fidia muathirika ya Sh 500,000.