Airbus A220 ya ATCL yarejea nchini

SERIKALI imebainisha kuwa ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) iliyokuwa inashikiliwa nchini Uholanzi kwa sababu za kisheria, imesharejea nchini tayari kwa kuendelea na kazi.
Pamoja na hayo, imeelezwa kuwa kutokana na mvua nyingi zilizonyesha hivi karibuni bwawa la mradi wa Julius Nyerere limeingia maji mengi na kama hali itaendelea hivyo, majaribio ya kuzalisha umeme yatafanyika Februari badala ya Aprili mwakani.
Hayo yalielezwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha kuhusu Tanzania kuwa Mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Mapambano ya Rushwa Afrika yanayofanyika kila mwaka Julai 11. Maadhimisho hayo yanaanza leo na kilele chake kitahudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan keshokutwa.
Akizungumzia bajeti ya mwaka huu ya 2023/2024 iliyopitishwa na Bunge la 11 iliyokwisha anza, alieleza kuwa anazo habari njema kwamba ndege ya ATCL iliyokuwa inashikiliwa Uholanzi kwa sababu za kisheria imekwishawasili nchini.
Akizungumzia ripoti ya CAG kuhusu shirika la ATCL kupata hasara kila mwaka, alikiri kuwa ni kweli linapata hasara kutokana na hali yake mbaya iliyokuwa awali, lakini kadri serikali inavyoendelea kuliboresha ndivyo hasara hiyo inavyozidi kupungua.
Alisema serikali kupitia shirika hilo, inategemea kufanya biashara kubwa ya utalii. “Huwezi kuwa na watalii kama huna ndege za kutosha. Hizi bilioni 217 sehemu kubwa zinakwenda kwenye ununuzi wa ndege. Leo ATCL inaruka vituo zaidi ya 15 nchini na sita nje ya nchi. Kote watatuletea watalii,” alieleza.
Akizungumzia uzalishaji umeme wa kutosha nchini alisema kupitia mradi wa umeme wa Julius Nyerere katika mto Rufiji kwenye bajeti ya mwaka huu imetengwa Sh trilioni 1.5 kwa ajili ya kumalizia mradi huo.
“Hivi ninavyozungumza kazi ya ujazaji maji inaendelea kwenye kiwango kilichopangwa cha kufika mita 163 juu ya usawa wa bahari. Tulitarajia pengine tungejaza kwa misimu miwili au mitatu lakini Mungu si Athumani, umekuja msimu mmoja tu maji yameshajaa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa wataalamu hali hiyo ikiendelea bwawa hilo linaweza kufika hata mita 184 ifikapo Januari, mwakani.
Pia, kwenye bajeti serikali imetenga fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa kusindika gesi asilia na kimiminika (LNG).
Akizungumzia maadhimisho ya siku ya kupambana na rushwa alisema leo yatafunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kutakuwa na matembezi ya amani na mabanda ya maonesho ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Kuzuia Uhujumu Uchumi Zanzibar.