Airtel yajivunia mapato

Matumizi ya intaneti na huduma za fedha kupitia simu yamekuwa injini kuu ya ukuaji wa Airtel Africa, huku kampuni hiyo ikitangaza ongezeko kubwa la mapato na faida kwa mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2026.
Airtel Africa imesema faida halisi imepanda zaidi ya mara mbili hadi dola milioni 813, kutoka dola milioni 328 mwaka uliopita. Ongezeko hilo limetokana na ukuaji wa mapato ya uendeshaji na faida za ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Mapato ya kampuni yamepanda kwa asilimia 29.5 kufikia *dola bilioni 6.42 Kwa sarafu thabiti, ukuaji huo ni asilimia 24.
Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema matokeo hayo yanaonyesha “msingi imara wa biashara na utekelezaji wenye nidhamu,” na kwamba matumizi ya huduma za kidijitali na uwekezaji wa mtandao ndiyo nguzo kuu za ukuaji.
“Mkakati wetu umeleta ongezeko la rekodi la wateja, mapato na faida kabla ya kodi na riba (EBITDA). Data na huduma za fedha mtandao ni injini muhimu ya ukuaji wetu katika kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali barani Afrika,” alisema Taldar.
Data na Airtel Money zinatawala
Idadi ya wateja wa Airtel Africa imeongezeka kwa *asilimia 10.5* hadi *milioni 183.5* – ongezeko kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa na kampuni.
Wateja wa huduma za data wamefikia *milioni 84.2*, huku matumizi ya simu janja yakipanda hadi *asilimia 49.5*. Matokeo yake, matumizi ya data kwa kila mteja yamepanda hadi *GB 8.9 kwa mwezi* kutoka GB 7.0 mwaka uliopita. Mapato ya data yamepanda kwa *asilimia 35.2* kwa sarafu thabiti na sasa ni chanzo kikuu cha mapato.
Huduma za *Airtel Money* nazo zimekua kwa kasi. Wateja wameongezeka kwa *asilimia 21.3* kufikia *milioni 54.1*, huku thamani ya miamala kwa mwaka ikipanda *asilimia 49* na kufikia zaidi ya *dola bilioni 215* katika robo ya nne pekee. Mapato ya Airtel Money yamepanda kwa *asilimia 28.4* kwa sarafu thabiti, yakiendeshwa na malipo ya kidijitali, huduma za wafanyabiashara na miamala ya kimataifa.
Uwekezaji na mtandao
Faida kabla ya riba, kodi na makato (EBITDA) imepanda kwa *asilimia 30.4* hadi *dola bilioni 3.16*, huku kiwango cha faida kikifikia *asilimia 49.3*. Faida ya uendeshaji imepanda *asilimia 45.1* hadi dola bilioni 2.12, na faida kwa kila hisa (EPS) imepanda hadi *senti 18.6* kutoka senti 6.0.
Uwekezaji wa mtaji umeongezeka *asilimia 31.9* hadi *dola milioni 884*, ukilenga upanuzi wa mtandao. Kampuni imejenga vituo vipya *3,250* na kuongeza *kilomita 3,200* za nyaya za fiber. Mtandao wa 4G sasa unapatikana katika *asilimia 98.5* ya vituo vyote, na vituo *3,100* vya 5G vinafanya kazi katika masoko sita.
Airtel inatarajia kuongeza uwekezaji hadi *dola bilioni 1.1* mwaka wa fedha 2027 ili kuimarisha miundombinu ya kidijitali na mtandao wa kasi.
Kampuni pia inapanua ushirikiano wa kimkakati, ikiwemo mradi wa mawasiliano ya satelaiti na SpaceX kupitia Starlink Direct-to-Cell, ili kufikisha huduma vijijini visivyo na mtandao wa kawaida.
Airtel Africa inasema mahitaji ya huduma za kidijitali bado yako juu katika masoko yake 14, licha ya changamoto za mfumuko wa bei na mabadiliko ya sarafu, hususan Nigeria.



