DAR ES SALAAM : MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amethibitisha kutokea kwa ajali ya lori kuhama njia na kuparamia kituo cha bodaboda kilichopo Kimara Stop Over usiku wa kuamkia leo, Februari 14, 2025 na kuua watu watatu.
Lori hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam, ambapo katika ajali hiyo, Chalamila amesema hadi saa 9:00 alfajiri, miili mitatu iliyokuwa imekandamizwa na kontena la lori hilo imeshatolewa.
“Miili ya watu hawa inasemekana walikuwa madereva pikipiki. Pia tumefanikiwa kutoa pikipiki nyingi zaidi kuliko watu tuliowakuta, na kwa mantiki hiyo, taarifa rasmi kutoka kwa Polisi itaweka bayana,” amesema Chalamila. SOMA : Gari lililobeba mirungi lapata ajali, mmoja afariki
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, RPC Mtatiro Kitinkwi, amesema kuwa kutokana na idadi ya pikipiki kuwa kubwa kuliko miili iliyokutwa, inawezekana wakati wa tukio, watu walikimbia ili kujiokoa.
“Taarifa kamili tutaitoa punde tutakapojua chanzo cha ajali hii, kwani imetokea usiku na tumekuwa hapa kwa zaidi ya saa mbili,” amesema Kitinkwi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wanasema makondakta wa gari lililosababisha ajali wanasema dereva alikuwa anasinzia toka wakiwa Mbezi na wakamwambia asimamishe gari alale lakini dereva akagoma ndio wakajikuta imetokea ajali hiyo.