WAFANYAKAZI watano kati ya nane wa Shirika la Menejimenti na Maendeleo ya Afya (MDH) waliokuwa wakisafiri kwa ndege ya Precision Air iliyoanguka Ziwa Victoria Jumapili wamefariki Dunia.
Walikuwa wanaelekea Tabora kufanya tathmini ya mwaka ya programu za shirika hilo, HabariLEO linaripoti.
Akizungumza na HabariLEO kwa njia ya simu Jumapili usiku, Ofisa Mtendaji Mkuu wa MDH, Dk David Sando ameeleza kuwa watumishi hao walianza safari Dar es Salaam lakini walilazimika kusafiri na Ndege ya Kampuni ya Precision Air hadi Bukoba kisha waende Mwanza ndipo waweze kuunganisha safari ya Tabora.
Hali hiyo imetokana na kubadilika kwa ratiba ya ndege.
k
Gazeti la HabariLEO lilivyoripoti kwa kina juu ya ajali hiyo Kwa mujibu wa Dk Sando, wafanyakazi watano wa MDH waliofariki katika ajali hiyo ni wabobezi katika masuala ya afya ya jamii.
Hadi jana Jumapili, taarifa rasmi zilionesha kuwa jumla ya watu 19 walikuwa wamethibitika kufariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea baada ya ndege hiyo yenye usajili 5H-PWF, ATR42-500 kushindwa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba Jumapili, Novemba 6, mwaka huu.
Wafanyakazi watatu wa MDH ni miongoni mwa watu 26 waliookolewa katika ajali hiyo, shukrani kwa juhudi zilizofanywa na wavivu katika ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika.
Ndege hiyo iliondoka Dar es Salaam Jumapili alfajiri kwenda Buboba ikiwa na watu 43 wakiwamo abiria 39 na wafanyakazi wanne. Miongoni mwa wafanyakazi hao ni rubani pamoja na msaidizi wake.
“Tumeshawasiliana na wafanyakazi wote na kesho [Jumatatu] taarifa rasmi itatolewa juu ya hili,” alisema mtendaji huyo huku akiongeza kuwa MDH inaendelea kushirikiana na familia za wafiwa katika maandalizi ya kupumzisha miili ya wafanyakazi hao.
Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa wa watu mashuhuri waliotuma salamu za rambirambi baada ya kutokea ajali hiyo.
Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya ndege ya Shirika la Precision katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera. Natuma salamu za pole kwa wote walioathirika na ajali hii. Tuendelee kuwa watulivu wakati huu zoezi la uokoaji likiendelea huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusaidie.
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) November 6, 2022
Hadi anazungumza na HabariLeo Jumapili usiku, Dk Sando alisema miili ya watumishi hao ilikuwa bado imehifadhiwa mjini Bukoba.
Majina ya watumishi watano wa MDH waliofariki katika ajali hiyo ni Dk Boniface Jullu, Dk Neema Faraja na Dk Alice Simwinga pamoja, Sauli Epimark na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano MDH Zacharia Mlacha.
Walionusurika ni Nickson Jackson, Dk Josephine Mwakisambwe na Dk Felix Otieno.
Chanzo cha kuaminika katika Shirika la MDH kimeeleza baadhi ya wafanyakazi walishindwa kusafiri na ndege hiyo kutoka Dar es Salaam baada ya kujaa hivyo huenda maafa zaidi kwa watumishi wao yangeongezeka.