‘Usawa kijinsia nguzo muhimu maendeleo endelevu’

DAR ES SALAAM: Imeelezwa kuwa usawa wa kijinsia unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu, kukuza uchumi na kuimarisha utawala bora ndani ya jamii na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Jinsia Duniani yaliyofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), yaliyopewa jina la CBE Gender Day.

Katika hafla hiyo, ameipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia sera, mifumo na programu mbalimbali.
Fatma amesema juhudi hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia unapaswa kupewa kipaumbele katika sekta zote ili kufikia maendeleo jumuishi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga, amesema uongozi wa chuo hicho umeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanawake kwa kuwapa fursa za kiuongozi na kitaaluma.

Naye mtoa mada, Lulu Mahai, amesema hatua mbalimbali zinazochukuliwa na chuo hicho, ikiwemo kuanzishwa kwa dawati la jinsia, utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, zimeendelea kuwa chachu ya maendeleo ndani ya taasisi hiyo.



