Ajali yaua watu wawili akiwemo dereva

Ajali yaua watu wawili akiwemo dereva

WATU wawili wamekufa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace kuligonga lori kwa nyuma katika eneo la Kwedizinga wilayani Handeni katika Mkoa wa Tanga.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Sofia Jongo alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 12 asubuhi wakati basi hilo dogo lilipotaka kulipita lori eneo lisilostahili, dereva alishindwa kulimudu gari akaligonga lori kwa nyuma.

Kamanda Jongo alisema katika ajali hiyo alikufa dereva wa basi hilo dogo na abiria mmoja.

Advertisement

“Dereva huyo aliwapita polisi akiwa na mwendo wa kawaida ila mbele kumbe aliongeza mwendo na kusababisha kutokea ajali wakiwa wanapanda mlima uliopo eneo hilo ambalo kuna kona kali,” alisema.

Kamanda Jongo alisema eneo hilo hutokea ajali za mara kwa mara kwa sababu watumiaji wa barabara wamekuwa wakitii sheria wanapowaona polisi ila wakishawapita huongeza mwendo.