Ajira mpya uwalimu kufanya mtihani

Serikali yasema mbali na mtihani usahili upo pale pale

SERIKALI imetangaza utaratibu wa ajira mpya za walimu na kwamba ili kuajiriwa ni lazima ufanye mtihani na atakaefaulu ndio atafanya usahili wa kazi.
Utaratibu huo mpya umetangazwa rasmi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda katika hafla ya kukabidhi tuzo za walimu iliyofanyika kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya  CRDB, Upanga jijini Dar es Salaam.
Mkenda amesema kuzungumzia ubora wa elimu  bila walimu bora na wazuri ni kazi bure.
“Malalamiko mengi elimu yetu ipo shagalabagala, lakini pamoja na mapungufu kwenye elimu yetu wapo walimu Wazuri  ambao kama nyie (walioshinda tuzo)  mnatia moyo.
“Tunataka kurudisha heshima ya walimu, kwenye jamii waliheshimika, walitumika kutatua migogoro kwenye jamii, walisikilizwa, tulipojikwaa tunataka kusawazisha, turudi kule kama zamani, kwa Ualimu unachukuliwa kama chaguo la mwisho.
“Kwa sasa, ajira ya ualimu inahusisha kutuma maombi katika tovuti maalum ya maombi ya ajira, kisha anayepata nafasi hufanyiwa usaili kisha kupangiwa eneo la kazi.
“Sera mpya ya elimu itaendeleza mafunzo kazini, itasisitiza fursa za walimu za kusoma.”Amesema na kuongeza
“Lakini kwa walimu wa wapya, tutachukua wazuri kwenda Ualimu watakaobaki waende kwenye kazi nyingine, tutachukua ‘the best’, tukitangaza nafasi za kazi ili  kupata  utafanya mtihani, haijalishi umesoma na unaufaulu mzuri kiasi gani, itatuondolea matatizo.
“Hakutakuwa na vimemo wala ‘connection’, hatutaangalia ni mtoto wa nani, na mbali na mitihani watafanya ‘interview’ vile vile kama kawaida….; “
“Tunataka iwe kama udaktari tu.”
Aidha, Mkenda amesema somo la biashara litakua ni la lazima na litafundishwa kwa vitendo ili kuwaandaa wanafunzi kujiajiri.
Hata hivyo, Mkenda amekiri upungufu wa walimu wa masomo hayo na kudai kuwa serikali inashughulikia ili kupunguza uhaba wa walimu masomo hayo.
Nae,  Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba akizungumza tuzo za walimu amesema tuzo zilizotolewa kwa walimu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa BUST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Amesema, shindano hilo lilianza Aprili mwaka huu na video za walimu kutoka halmashauri 26 zilikusanywa zikiwa na maudhui ya kufundisha Hesabu na kuhesabu.
“Shindano hilo liliwalenga walimu wa awali na msingi wanaofundisha kuhesabu na hisabati. Mahiri za kufundisha za kufundisha zilizochaguliwa ni Geometri, Aljebra, namba kamili na takwimu,” amesema.
Umahiri wa matumizi ya teknolojia, mawasiliano mazuri na wanafunzi, mbinu za kushawishi wanafunzi kupenda somo ni miongoni mwa vigezo vilivyoangaliwa.
DK Komba amevitaja vigezo vingine ni tathmini ya kupima iwapo wanafunzi wameelewa, huku Mei 22 ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho ya kupokea kazi.
Kwa mujibu wa Dk Komba, video 99 zilikusanywa na kufanyiwa tathmini kwa awamu tatu hadi kupatikana video 18.

Habari Zifananazo

Back to top button