Akayabangu, vumbi la kongo ni Viagra, zapigwa marufuku

WIZARA ya Afya kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limepiga marufuku dawa ya kuongeza nguvu za kiume maarufu Akayabangu.

Taarifa ya Wizara ya Afya iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Profesa Hamis Malebo imesema kuwa dawa hiyo haijathibitishwa na baada ya uchunguzi wamebaini inachanganywa na Viagra.

Amesema, baraza lilipokea taarifa ya uwepo wa dawa hiyo sokoni na hivyo ikafanya uchunguzi wa uingizwaji, usambazaji, ubora na usalama wa kinywaji hicho..

Amesema, baada ya  uchunguzi imegundulika kuwa, kinywaji hicho hakijawahi kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

“Kinywaji hicho cha Akayabangu kimechanganywa na dawa ya kisasa aina ya Sildenafil (Viagra majina mengine Erecto ama Vega) jambo ambalo ni kinyume cha Sheria.”Amesema Profesa Malebo

Amesema kutokana na hali hiyo, hicho siyo kinywaji cha tiba asili bali ni kinywaji chenye viagra.

” Baraza linapiga marufuku uingizaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa kinywaji hiki kote nchini.

“Yeyote atakayekiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na atakayepatikana akiwa na kinywaji cha Akayabagu, atakuwa ametenda kosa na ataweza kushitakiwa kwa mujibu wa Sheria,” amesema Profesa Malebo.

Aidha, amesema baraza lina tahadharisha umma kuwa makini na matumizi ya dawa ambazo hazijasajiliwa kama Akayabangu  na vumbi la kongo kwani dawa hizo hazijapimwa ubora na usalama wake na mamlaka zinazotambulika kisheria.

Amesema pia, kuanzia leo baraza linapiga marufuku uingizaji,usambazaji, uuzaji na utumiaji wa vumbi la Kongo kote nchini.

“Yeyote atakayekiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Pia ikumbukwe kuwa, yeyote atakayepatikana akiwa na vumbi la Kongo atakuwa ametenda kosa na atashitakiwa kwa mujibu wa Sheria.

“Mtumiaji anayo haki ya kuuliza na kufahamishwa taarifa ya dawa anazopewa kutumia na kuomba kuoneshwa cheti cha usajili wa dawa hizo.

Baraza linaendelea kuikumbusha jamii kuacha tabia ya kutumia dawa hovyo kwani iwapo dawa sio bora na salama, zinaweza kuleta madhara ya kiafya kwa mtumiaji,” amesema Profesa

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button