Akinamama wakacha kliniki, wajijazia kadi

BAADHI ya akinamama wa Wilaya ya Mbeya wanadaiwa kujaza kadi za kliniki zinazoonesha maendeleo ya mtoto badala ya jukumu hilo kufanywa na wataalamu wa afya jambo ambalo limekua chanzo cha tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri ya chini ya miaka mitano.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na watoa huduma ya mama na mtoto kutoka Hospitali teule ya Ifisi iliyopo mji mdogo wa Mbalizi wakati wakitoa chanjo na elimu ya lishe na uzazi kwa akinamama katika Kituo cha Hope kinachojihusisha na masula ya watoto na watu wenye mahitaji maalumu.

Ofisa Muuguzi msaidizi kutoka Hospitali ya Mbalizi, Heriet Mwasenga alisema mama anapohudhuria kliniki anapata elimu ikiwemo uzazi wa mpango, chanjo, lishe na ushauri kulingana na maendeleo ya mtoto hivyo kitendo cha mama kujaza kadi kunaleta athari kubwa katika ukuaji wa mtoto.

Muuguzi kutoka Hospitali ya Ifisi, Leah Mwakasungura alisema tatizo hilo lipo katika kituo chao hivyo wameongeza mikakati ya kutoa elimu ya afya kwa akinamama kila wanapohudhuria kliniki ili kukabiliana na matatizo kwa watoto ikiwemo udumavu.

Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Sauti ya Mama Afrika(SAMAFO), Tabitha Bugali alisema kwa kushirikiana na hospitali hiyo wamekutana na akinamama zaidi ya 80 kwa lengo la kutoa elimu kuhusu mtoto  ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha malezi bora kwa watoto kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Kuruthum Mbekaye alisema kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika wamejipanga kuelimisha wazazi na walezi kuhusu malezi bora kwa watoto, huku akitoa tahadhari kwa wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao katika kipindi hiki cha likizo ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili.

Naye Mratibu wa kituo cha Hope, Musa Simyenga alisema jamii inapaswa kuondokana na kukaa kimya na taarifa za matukio ya ukatili ikiwemo wazazi kumalizana nyumbani kwani tabia hiyo hukwamisha juhudi za kutokomeza matukio ya ukatili na kuwaathiri watoto na kutowatendea haki.

Habari Zifananazo

Back to top button